Aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Kahama, James Lembeli ameelezea
kinachoendelea katika maisha yake ya kisiasa hasa baada ya kushindwa
katika uchaguzi wa mwaka huu akiwa ndani ya chama chake kipya cha
Chadema.
Akiongea katika taarifa rasmi kwa wananchi wa jimbo hilo, Lembeli
amesema kuwa hivi sasa atajikita zaidi katika shughuli za chama chake
pamoja na shughuli alizokuwa akizifanya kabla ya kuwa mbunge wa jimbo
hilo.
Alisema kuwa ataendelea kufanya kazi zake na mashirika ya kimataifa kama
mjumbe wa Bodi mbalimbali. Pia, ataendelea kufanya kazi ya kusimamia
radio yake (Kahama FM) ambayo amedai kuwa taarifa zilizosambazwa kuwa
ameiuza kulipa deni la mkopo aliopewa kuendesha kampeni sio za kweli.
Pia, Lembeli amewashukuru wananchi waliojitokeza kumuunga mkono na
kuahidi kuendelea kushirikiana nao katika masuala ya maendeleo na
ataendeelea kushirikiana nao kukamilisha miradi mbalimbali aliyokuwa
ameanza kuitekeleza kwa juhudi zake binafsi.
Kadhalika, Lembeli amekanusha taarifa zilizokuwa zimesambazwa kuwa
alikamatwa na jeshi la polisi mara tu baada ya Jumanne Kishimba wa CCM
kutangazwa kuwa mshindi.
Kuhusu afya yake, alisema kuwa yeye ni mzima tofauti na habari
zinazoendelea kuenea kuwa ni mgonjwa hasa baada ya kupata ajali ya gari
na matokeo kutangazwa
Tagged with: SIASA
Hakuna maoni :