Aliyekuwa
Kocha wa Taifa Stars, Mdenishi, Kim Poulsen, amefunguka kuwa yupo
tayari kuchukua mikoba ya Muingereza, Dylan Kerr ya kuifundisha Simba
endapo viongozi wa klabu hiyo watamfuata na kuzungumza naye juu ya dili
hilo.
Hivi
karibuni Simba ilifikia uamuzi wa kuachana na Kerr baada ya timu hiyo
kuwa na mwenendo mbaya katika Ligi Kuu Bara pia kufanya vibaya kwenye
Kombe la Mapinduzi.
Poulsen
ambaye amekuja nchini kwa ajili ya mapumziko, tangu awasili wiki
iliyopita amekuwa akienda uwanjani kuangalia mechi mbalimbali za ligi
kuu huku akionekana kuwa makini na ‘kunoti’ baadhi ya matukio ya
uwanjani.
Kocha
huyo mwenye miaka 56, aliwahi kufundisha timu za vijana za Tanzania
kuanzia mwaka 2011 mpaka 2012, kabla ya kukabidhiwa mikoba ya kuinoa
Taifa Stars mwaka 2012 mpaka 2014.
Awali
Simba ilikuwa ikimuhitaji kocha huyo aweze kuifundisha timu yao baada ya
kuachana na Mserbia Goran Kopunovic, msimu uliopita, lakini mambo
hayakuenda vizuri na kumpa Kerr jukumu hilo.
Akizungumzia
ishu ya kuinoa Simba, Poulsen alisema wakati anaondoka Tanzania mwaka
2014, alitamani siku moja arudi nchini kama kocha na sasa amepata nafasi
ya kuja kwa ajili ya mapumziko, hivyo hatakataa kama akifuatwa na
viongozi wa Simba na kutakiwa kupewa mikoba ya kuinoa timu hiyo
iliyoachana na Kerr wiki moja iliyopita.
“Kwa
nini nikatae, nipo tayari kwa hilo kwani wakati naondoka hapa nchini
baada ya kuachana na Stars nilitamani kurudi tena nikiwa kocha.
“Nimekaa
Tanzania kwa miaka mitatu, hivyo nataka kufundisha tena hapa nchini,
japo kwa sasa nimekuja kwa ajili ya mapumziko na mwishoni mwa mwezi huu
natarajia kurudi nyumbani Denmark kuendelea na shughuli zangu, lakini
nimekuwa nikienda uwanjani kuangalia baadhi ya mechi za ligi.
“Katika
mechi nilizozishuhudia mpaka sasa, nimeziona Simba, Yanga na Azam
zikicheza lakini siwezi kuongelea chochote juu ya ‘pafomansi’ zao kwani
ni mapema mno, nahitaji kuziona zaidi na zaidi.
“Kesho
(leo) kuna mechi za ligi tena, Simba itakuwa nyumbani (Uwanja wa Taifa,
Dar) na Azam ugenini (Mkwakwani, Tanga), nitaenda kuiangalia Simba
ikicheza lakini pia Yanga itakapocheza (kesho Alhamisi katika Uwanja wa
Taifa) nitaenda pia,” alisema Poulsen.
Hakuna maoni :