Sisi,
viongozi wa Dini pamoja na taasisi zinazosimamia mchakato wa uchaguzi
(NEC, TAKUKURU, Polisi pamoja na Msajili wa vyama vya
siasa) tuliokutana leo tarehe 17/9/2015, tumepata nafasi ya kujadili
kwa kina suala la uhuru,haki na amani kuelekea uchaguzi mkuu
utakaofanyika 25/10/2015 na wajibu wa kila mdau kuhakikisha kuwa
uhuru,haki na amani vinalindwa kipindi hiki.
Suala
la uhuru haki na amani ni wajibu wetu sisi viongozi wa dini na
watanzania wote kwa ujumla na halina mjadala.Kila mmoja achukuwe nafasi
yake kulinda uhuru,haki na amani na kuweka uzalendo kwanza kuliko
kutanguliza maslahi binafsi ya vyama vya siasa.
Viongozi
wa dini wamepata nafasi ya kujadili na vyombo hivi masuala ya msingi
kama kuhakikisha kuwa maadili ya uchaguzi yanazingatiwa kwa wote, muda
wa kutangaza matokeo ya kura unazingatiwa , haki ya wananchi kupata
matokeo haraka ili kuepuka fujo wakati wa kusubiri na kutangazwa kwa
matokeo.
Jeshi
la polisi kutokutumia nguvu kupita kiasi, wajibu wa Msajili kuhakikisha
vyama vyote vinapata fursa sawa na pia tumejadili suala la kutumia
nyumba za ibada kama sehemu ya jukwaa la siasa.
Viongozi
wa dini tumekubaliana kwa pamoja kuepuka kutumia nyumba za ibada
kuonyesha ushabiki wa aina yoyote kwa chama chochote cha siasa.
Baada ya kujadili kwa kina masuala hayo viongozi wa dini wanatoa wito ufuatao;
1. Vyombo vya habari vifanye kazi kwa ueledi bila upendeleo na pia kuhakikisha kuwa inatoa taarifa ya kutosha kuelimisha umma.
2.
Tunaishauri NEC kwenye chaguzi zijazo iweke utaratibu maalum wa
kuruhusu wanafunzi wa vyuo vikuu waliojiandikisha pamoja na watu wote
waliojiandikisha/ watakaojiandikisha waweze kupiga kura.
3. Tunaishauri NEC kwenye chaguzi zijazo siku ya kupiga kura isiwe siku ya ibada.
4.
NEC iendelee kutoa elimu ya uraia kuhusu haki ya raia kupiga kura na
haki yao ya kukaa mita mia moja kusubiri matokeo yatangazwe kwa utulivu
kama ambavyo NEC imehakikishia viongozi wa dini kuwa kila kituo
itabandika matokeo yote (Urais,Ubunge na Udiwani)
5. Pamoja
na kutimiza wajibu wake wa msingi wa kulinda raia na mali zao Jeshi la
polisi wakati huu wa uchaguzi liendelee kutimiza wajibu wake wa
kusimamia amani na taratibu kwa haki bila upendeleo.
6.
Wagombea,wafuasi na wanaowanadi, wanaaswa waache mara moja lugha za
matusi,vitisho,kejeli na kukashifiana vinavyoweza kuchochea fujo na
kuleta uvunjifu wa amani wajikite kunadi sera za vyama vyao.
7.Tunawahimiza
wananchi kuwa makini katika kufuatilia kampeni na sera mbalimbali za
wagombea, kuzipima kwa hali ya juu sera hizo, kutokuuza kadi zao za
kupigia kura, kutokununuliwa na kujitokeza kwa wingi kutumia uhuru na
haki yao ya kuchagua viongozi wanao wataka kwa hiari na amani.
8.
Viongozi wa dini wanawahimiza Watanzania wote kuendelea kuombea nchi
hii kuendelea kuwa taifa lililojengwa katika misingi ya uhuru , haki
na amani.
9.
Viongozi wa dini tutabaki kuwa manabii na wahubiri wa uhuru,haki na
amani wakati huu , wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi
Sisi
viongozi wa dini Tunawashukuru Inspekta generali wa polisi, Mwenyekiti
wa Tume ya Uchaguzi, Msajili wa Vyama vya siasa na Mkurugenzi Mkuu wa
TAKUKURU kwa ufafanuzi makini na wa kina juu ya nafasi na utayari wao wa
kushirikiana na viongozi wa dini kuhakikisha uhuru, haki na amani
vinaendelea nchini.
Maelezo
yao na mafafanuzi yao tumeyasikia na tutaendeleza kwa kuwa hiki ni
kikao cha mwanzo na tutaendelea kuwa na vikao vingine pamoja nao
kuelekea uchaguzi mkuu ili kufuatilia utekelezaji na kuendeleza
makubaliano yetu katika kuhakikisha uhuru,haki na amani.

Hakuna maoni :