KLABU
Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imefanya usajili kwa
nafasi moja na kuwatoa kwa mkopo wachezaji wengine wanne katika dirisha
dogo la usajili lililofungwa nchini saa 6.00 usiku wa kuamkia leo.
Akizungumza na mtandao wa azamfc.co.tz, Makamu Mwenyekiti wa Azam FC, Nassor Idrissa ‘Father’, alisema mchezaji pekee ambaye wamemsajili ni kipa, Ivo Mapunda.
Usajili
wa kipa huyo wa zamani wa Tanzania Prisons, Yanga, St. Georges ya
Ethiopia, Gor Mahia ya Kenya na Simba, ni sehemu ya mapendekezo ya
benchi la ufundi la Azam FC katika kuipa nguvu sehemu ya langoni yenye
makipa wengine Aishi Manula na Mwadini Ali.
Benchi
la Ufundi chini ya Stewart Hall, limesema kuwa makipa hao watatu
watatosha kukabiliana vema na wingi wa michuano iliyo mbele yao, Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL), Kombe la Mapinduzi, Kombe la FA (Azam Sports
Confederation) na Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.
“Lakini
kuna vijana wetu wadogo wadogo wanne tmewapeleka kwa mkopo timu
nyingine wakapate nafasi ya kucheza na wataanza kucheza mara baada ya
taratibu zote za usajili kumalizwa na Kamati ya Usajili na Hadhi za
Wachezaji,” alisema.
Wachezaji
hao wanaoondoka kwa mkopo ni beki Ismail Gambo 'Kussi' aliyeelekea
Mwadui ya Shinyanga, kiungo Bryson Raphael amekwenda Ndanda ya Mtwara,
kiungo Omary Wayne ametua Coastal Union ya Tanga, huku winga Kelvin
Friday akichukuliwa na Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Akitolea
ufafanuzi wa suala la Kelvin Friday kwenda Mtibwa, wakati anatakiwa
kwenye majaribio katika timu ya St. Georges ya Ethiopia, Father alisema
wameamua kufanya hivyo ili kuwahi muda wa usajili wa Tanzania uliofungwa
jana na atakwenda huko mambo yakiwa yameshakamilika.
“Kipindi
chake cha kwenda kwenye majaribio kipo mbele na dirisha letu la usajili
limefungwa jana, tumempeleka huko ili aendelee kucheza wakati
akisubiria mambo yake ya kwenda huko kukamilika bahati nzuri kocha
aliyemuomba ni Mart Nooij, aliyewahi kuwa Kocha Taifa Stars,” alisema.
Father
aliongeza kuwa: “Tayari hivi sasa tumeshatuma passport yake, nyaraka
zake kwa ajili ya kumuombea viza, mambo yote hayo yakishakamilika
atakwenda mara moja na akifaulu majaribio klabu zote mbili tutakaa chini
na kukubaliana. Sisi tunaamini ya kuwa atafaulu na mambo mengine
kuendelea.”
Friday,
20, anatakiwa na mabingwa hao wa Ethiopia kwa majaribio ya muda wa wiki
moja n tayari uongozi wa Azam FC umepokea kwa mikono miwili suala hilo
na umempa baraka zote za kwenda huko mambo yakishakamilika.
Hakuna maoni :