Mgombea ubunge wa Kigoma Kusini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, David
Kafulila ameanguka katika matokeo yaliyotangazwa jana jioni dhidi ya
mpinzani wake wa CCM, Hasna Mwilima.
Akitangaza matokeo hayo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Uvinza ambaye pia
ndiye Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kigoma Kusini, Ruben Mfume
amesema Kafulila alipata kura 33, 382 huku mpinzani wake wa CCM akipata
kura 34, 453.
Akizungumzia kuchelewa kutangazwa kwa matokeo katika jimbo hilo, Mfume
amesema ni kutokana na kuwepo malalamiko kadhaa toka kwa wagombea wote
wawili wa CCM na NCCR-Mageuzi ambapo mgombea wa CCM alikuwa anataka kura
zihesabiwe upya.
Mfume amesema, mgombea wa CCM (Mwilima) alitoa madai kuwa fomu zake za
kurekodi matokeo zilionekana zimefutwafutwa kwenye kata nyingi, hali
iliyompa wasiwasi kuwa huenda matokeo yake kwenye Kata hizo yamechezewa.
Katika madai mengine, Mfume amesema Mwilima amedai fomu zake za matokeo
kwenye kata nyingi zilionekana kusainiwa na mawakala wa chama cha
mpinzani wake (NCCR-Mageuzi), hali iliyomuondolea imani ya usahihi
takwimu za matokeo hayo.
Kwa upande wake, Kafulila amepinga hoja ya kutaka kura zihesabiwe upya
kwa madai kuwa hakuwa na imani na waliopewa dhamana ya kuzilinda kura
zao baada ya kuhesabiwa akidai walinzi pamoja wa mkurugenzi huyo ni
mawakala wa CCM katika uchaguzi.
Kafulila amesema kutokana na uwakala wao kwa CCM, walinzi pamoja na
mkurugenzi huyo walikuwa na uwezo wa kufanya lolote baada ya zoezi la
kuhesabu kura kukamilika na kubadili matokeo ili kuisaidia CCM kushinda.
Akizungumza baada ya matokeo kutangazwa, Kafulila amesema hakubaliani na
hatua ya mgombea wa CCM kutangazwa mshindi kwa kuwa dosari
walizolalamikia zilikuwa hazijapatiwa ufumbuzi wala yeye hakuwa
ameridhia matokeo hayo yatangazwe.
Matokeo ya udiwani katika jimbo hilo lenye Kata 16 yanaonyesha kuwa, CCM
kimeshinda Kata 13, vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema na ACT-Wazalendo
vikijipatia ushindi katika Kata moja kila kimoja.
Tagged with: SIASA
Hakuna maoni :