Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman
Mbowe, amefichua mazito baada ya kueleza hadharani kuwa kamwe chama
chake na washirika wao wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
hawatakubali matokeo ya uchaguzi mkuu yatakayobainika kuwa yamepikwa.
Kadhalika, alisema ni vyema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na mamlaka
za serikali iliyopo madarakani kuheshimu maamuzi ya wananchi
yatakayotokana na kura watakazopiga kwenye uchaguzi mkuu Jumapili ijayo,
kwani kinyume chake ni kuhatarisha amani iliyopo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana baada ya kutoa heshima za mwisho
kwa mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Dk. Emmanuel Makaidi
wa chama cha National League for Democracy (NLD) aliyefariki dunia wiki
iliyopita, Mbowe alisema watakubali matokeo ikiwa mchakato wote wa
uchaguzi utakuwa huru, wa haki na usiokuwa na chembe ya mizengwe katika
kila hatua.
Chadema na vyama vingine vinavyounda Ukawa vya Chama cha Wananchi (Cuf),
NCCR-Mageuzi na NLD, vimemsimamisha waziri mkuu wa zamani, Edward
Lowassa kuwa mgombea wao wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, huku pia wakishirikiana kusimamisha wagombea wa nafasi za
ubunge, udiwani na uwakilishi.
Akieleza zaidi, Mbowe aliyekuwa akijibu swali aliloulizwa na waandishi
kuhusu namna walivyojiandaa kupokea matokeo baada ya uchaguzi mkuu
Jumapili ijayo, alisema Ukawa itakuwa tayari kupokea matokeo
yatakayotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ikiwa wataridhika
kuwa hatua zote za kisheria na haki za mchakato wa uchaguzi huo kuanzia
katika kampeni hadi upigaji kura zimezingatiwa ipasavyo.
Aliongeza kuwa kinyume chake, wao (Ukawa) hawatakuwa tayari kupokea matokeo yatokanayo na hila za namna yoyote ile.
Akifafanua, Mbowe alisema Ukawa haiwezi kukataa matokeo kwa sababu ya
kushindwa katika uchaguzi, bali wanachoangalia ni kuzingatiwa kwa haki,
sheria na uwazi katika hatua zote za mchakato wa uchaguzi huo.
“Kupokea matokeo ni mchakato ambao unaanzia katika hatua za kampeni,
upigaji kura hadi wakati matokeo yanatangazwa. Siwezi kusema eti
tutakataa matokeo kwa sababu tu Nec imetangaza halafu tukaonekana
tumeshindwa… la hasha. Bali tutapokea matokeo kama haki, uwazi, sheria
na taratibu nyingine zimezingatiwa mpaka kupatikana kwa matokeo,”
alisema Mbowe na kuongeza:
“Sisi Chadema na Ukawa tunaamini kwamba wananchi watamchagua kiongozi
wanayemuamini. Lakini kama watu wengine wenye mamlaka ndani ya nchi
wakaamua kupindisha sheria na kupindisha maamuzi ya wananchi kupitia
sanduku la kura, kamwe hatutakubali matokeo hayo. Na hapo amani
tunayoihubiri inaweza kuwa ngumu ‘kui-control’ (kuidhibiti),” alisema.
Kuhusiana na mvutano juu ya wananchi kuondoka vituoni baada ya kupiga
kura na siyo kukaa mita 200 kutoka kwenye vituo vya kura, Mbowe alisema
msimao wao wa kulinda kura uko pale pale kwa kuwa wana amini kuwa hiyo
ni haki yao kisheria.
“Kura ni mali na kama hivyo ndivyo ni lazima tuilinde, tumepanga kulinda
kura zetu kwa amani na utulivu nje ya mita 200 kama sheria inavyosema…
tunaomba kila mtu na vyombo vya dola viheshimu,” alisema.
Aliongeza: “Kuhubiri amani bila haki ni kulishana upepo. Mamlaka zote za
taifa zina wajibu wa kuheshimu sheria za nchi na kuacha kutumia mamlaka
zao vibaya na bila vitisho. Kila mmoja akitekeleza wajibu wake kwa
misingi ya sheria, hiyo amani wala haitatafutwa, itapatikana tu.”
Mbali na Mbowe, wengine waliojitokeza katika shughuli ya kuuaga mwili wa
Dk. Makaidi ni Lowassa, Mgombea Mwenza wa Ukawa, Juma Duni Haji,
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia wa NCCR-Mageuzi , Waziri Mkuu
Mstaafu aliyehamia kambi ya Ukawa, Frederick Sumaye, Kaimu Katibu Mkuu
wa Cuf, Twaha Tasilima, Katibu Mkuu wa NLD, Tozzy Matwanga na Makamu
Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula.
Wengine waliokuwapo ni Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, mgombea ubunge wa Jimbo la Kawe, Halima Mdee.
Jaji Mkuu Ataka Mahakama Iachiwe Swala la Mita 200
Wakati Mbowe akisisitiza msimamo wa kuwataka wafuasi wa Ukawa kutorudi
nyumbani baada ya kupiga kura na badala yake kukaa umbali wa mita 200
kutoka vituo vya kupigia kura ili kulinda kura zao, Jaji Mkuu Othman
Chande alikataa kuzungumzia suala hilo na badala yake kutaka mahakama
iachiwe ili itoe uamuzi wake kwa haki.
Jaji Chande aliyasema hayo jana wakati alipoulizwa na waandishi baada ya
kufungua mafunzo kwa majaji na Wasajili Mahakama Kuu Jijini Dar es
Salaam, juu ya wajibu wa mahakama katika uchaguzi mkuu na namna ya
kukabiliana na changamoto zilizopo katika kusimamia kesi za uchaguzi,
yaliyoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC).
Tayari Mahakama Kuu imeshapanga majaji watatu kushughulikia suala hilo
lililoibua mvutano mkali hivi karibuni baina ya viongozi wa Ukawa na
wakuu wa Nec na Jeshi la Polisi. Kesi hiyo itaanza kunguruma rasmi leo.
Katika hatua nyingine, Jaji Chande alikiri kuwa uchaguzi wa mwaka huu ni
wenye mchuano mkali na kwamba mahakama zimejiandaa kumaliza kesi
zitakazotokana na uchaguzi huo kabla ya miezi sita inayotajwa kisheria.
Alisema mwaka 2010 kulikuwa na kesi 44 za uchaguzi kwa ngazi za Ubunge
na kati yake, 17 zilikwenda hadi hatua ya mwisho baada ya kutolewa
ushahidi huku nyingine zikiisha katika hatua za awali.
“Ushindani ni mkali katika uchaguzi huu, tunatarajia kupokea kesi nyingi
za uchaguzi. Tumejiandaa kupokea, kusikiliza kwa haraka ili kuwezesha
wapigakura kujua mshindi halali ni yupi,” alisema.
Akieleza zaidi, alisema sheria imeweka wazi kuwa anayestahili kufungua kesi siyo mpigakura bali wagombea wenyewe.
Mratibu THRDC, Onesmo Olengurumwa, alisema wameshirikiana na Ofisi ya
Jaji Kiongozi kuandaa mafunzo hayo kwa kutambua kuwa ni wadau muhimu
katika kushughulikia kesi za uchaguzi ili kuwezesha haki kutendeka kwa
haraka
Goodluck Jonathan Akiri Ushindani Ni Mkali Kati Ya CCM na UKAWA
Mkuu wa Jopo la Waangalizi kutoka Jumuiya ya Madola na aliyekuwa Rais wa
Nigeria, Goodluck Jonathan, amekiri kuwa uchaguzi wa mwaka huu nchini
Tanzania una ushindani mkali kutokana na namna vyama vilivyojiandaa
lakini akawataka wagombea wote wa nafasi za urais kujiandaa kukubali
matokeo kwa maslahi mapana ya taifa lao.
Wagombea wanaochuana kwa karibu ni, Dk. John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Lowassa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam mara baada
ya kuwasili nchini, Jonathan aliyekubali kuondoka madarakani Mei mwaka
huu na kumpisha Muhammad Buhari baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu
nchini mwake, alisema katika uchaguzi wowote kuna kushinda na kushindwa
na hivyo wagombea wajiandae kwa matokeo yoyote ili kuiacha nchi yao
ikiwa salama.
Alisema ijapokuwa ushindani ni mkali, Jumuiya ya Madola inaamini kuwa
uchaguzi utakuwa huru na haki na kwamba imani yao kubwa ni Tanzania
kusimamia demokrasia iliyokuwapo wakati wote tangu ipatre uhuru wake
mwaka 1961.
Jonathan anaongeza jopo lenye waangalizi 14 kutoka mataifa mbalimbali yaliyo wanachama wa Jumuiya ya Madola
Source:Mpekuzi blog
Tagged with: SIASA
Hakuna maoni :