HUKUMU ya rufaa iliyokatwa na waliokuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona, kupinga adhabu ya vifungo vya miaka mitatu jela inatolewa leo.
Jaji wa Mahakama Kuu, Projest Rugazia wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, anatarajiwa kusoma hukumu hiyo baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili.
Mahakama hiyo pia itatoa hukumu ya rufani iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu dhidi ya kina Mramba na wenzake.
Viongozi hao wa zamani kwa kupitia mawakili wao wamekata rufani Mahakama Kuu wakipinga adhabu ya vifungo walivyopewa na Mahakama ya Kisutu, baada ya kuwatia hatiani kwa matumizi mabaya ya madaraka kwa kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni ya ukaguzi wa madini ya dhahabu.
Julai 6 mwaka huu, Mahakama ya Kisutu ilitoa adhabu hiyo kwa Mramba na Yona baada ya kuwatia hatiani kwa matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7, kutokana na kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya Alex Stewart and Asseyers.
Katika hukumu hiyo, Mahakama ya Kisutu ilimwachia huru aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake.
Mramba na Yona kwa kupitia mawakili wao wanadai kwamba adhabu hiyo ni kubwa mno na hati ya mashtaka iliyowatia hatiani ilikuwa na upungufu wa sheria kama ilivyobainishwa katika kifungu namba 132 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Pia wanadai kwamba hapakuwapo ushahidi wa kutosha kuthibitisha mashitaka dhidi yao.
DPP anapinga adhabu waliyopewa mawaziri hao kwa madai kuwa ni ndogo.
Anadai hakimu alikosea kumuachia huru Mgonja kwa kigezo kwamba upande wa Jamhuri ulishindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yake.
Pia anadai Mahakama ya Kisutu ilikosea kutowaamuru Mramba na Yona kulipa hasara ya fedha waliyoisababishia serikali.
Hakuna maoni :