Joto la utawala wa Rais John Magufuli limebadili utendaji kazi wa
makatibu wakuu wa wizara mbalimbali waliozoea kukaa ofisini na sasa
wanafanya kazi nje ya ofisi na kusikiliza kero za wananchi kwenye maeneo
yao.
Wakati hilo likifanyika, Ikulu jijini Dar es Salaam imesema katibu mkuu
au mtumishi yeyote wa umma atakayeshindwa kwenda na kasi na mabadiliko
ya utendaji kazi katika serikali ya awamu ya tano ajiondoe.
Tamko hilo linalotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue,
alipohojiwa jana kuhusu kutokuwapo kwa makatibu wakuu wa wizara kadhaa
kwenye ofisini zao wiki iliyopita.
Makatibu wakuu wa Wizara kadhaa wamelazimika kuzifunga ofisi zao na kuelekea mikoani kusikiliza kero za wananchi.
Hali ya viongozi hao kuhama jiji na kwenda mikoani imeleta mabadiliko ya
utendaji kazi wao baada ya miaka ya nyuma kuzoeleka kutumia muda mwingi
ofisini na kuacha kazi za nje kufanywa na waziri, naibu au watendaji
wengine.
Baadhi ya wizara ambazo zilitembelewa na kukuta ofisi za katibu mkuu
zikiwa zimefungwa ni Uchukuzi, Tamisemi, Sayansi, Teknolojia na
Mawasiliano na Ujenzi.
Baadhi ya wafanyakazi wa wizara hizo ambao hawakutaka majina yao
yatajwe, walisema mabosi wao kwa sasa inakuwa nadra kuonekana ofisini
wakifanya kazi kwa kuogopa kuonekana wazembe.
"Hatujawahi kuona katibu anakwenda mikoani kama ilivyo sasa, kila siku
anakwenda huku na kule kuangalia miradi na kero za wananchi," alisema
mmoja wa wafanyakazi wa moja ya wizara hizo.
Hatuna Muda na Katibu Mkuu Goigoi-Sefue
Akitoa kauli ya serikali, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue,
alisema kuanzia sasa katibu Mkuu na mtendaji wa serikali ambaye anafanya
kazi kwa kusuasua ajiondoe mwenyewe.
Alisema tayari amefanya kikao na makatibu wote kuwaeleza suala hilo na
atakayerudi nyuma hatakuwa na nafasi katika serikali ya awamu ya tano.
"Jambo hilo tumekubaliana kwenye kikao, serikali ya awamu ya tano
haitakuwa na utani kwa wale watakaoonekana hawaendi na kasi ya Rais,
sasa wanatakiwa kuchagua kama wanataka kuendelea na nafasi zao au la,"
alisema Sefue
Tagged with: SIASA
Hakuna maoni :