Wakati saa 48 zilizotolewa na mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha
Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad kutaka Tume ya Uchaguzi
Zanzibar (ZEC) kuendelea na mchakato wa majumuisho ya kura na kumtangaza
mshindi wa urais wa Zanzibar zikiwa zimemalizika, Ikulu ya Jamhuri ya
Muungano imesema haijapokea maombi ya Maalim Seif kutaka kuonana na Rais
Jakaya Kikwete.
Ijumaa iliyopita, Maalim Seif aliwaambia waandishi wa habari visiwani
Zanzibar kuwa baada ya ZEC kufuta uchaguzi Jumanne iliyopita, alifanya
jitihada kadhaa za kuwasiliana na Rais Kikwete na pia Rais wa Zanzibar,
Dk. Ali Mohamed Shein, ili kuzungumzia suala hilo kwa maslahi ya
Zanzibar lakini wito wake huo umekuwa ukipuuzwa.
Maalim Seif alisema tangu kufutwa kwa uchaguzi, amefanya juhudi za
kutafuta ufumbuzi kwa kukaribisha mazungumzo na viongozi wenzake wa
kitaifa akiwamo Rais Kikwete na pia Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed
Shein, lakini wote wamekuwa wakimkwepa, licha ya kuanza kuwatafuta kwa
kutumia mawasiliano ya simu na ujumbe kupitia wasaidizi wao, akitaka
wakutane.
Hata hivyo, taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu
iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, ilieleza
kuwa Ikulu imesikitishwa na madai ya Maalim Seif, ikieleza kuwa siyo
kweli.
Badala yake, Ikulu imesema haijapokea ombi lolote kutoka kwa Maalim Seif
la kutaka kukutana na Rais Kikwete tangu siku ya kupiga kura na hata
baada ya Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, kufuta uchaguzi wa
Zanzibar.
Taarifa hiyo ya Ikulu imesema kile ambacho Rais Kikwete amekipokea ni
malalamiko ya CUF kuhusu baadhi ya vitendo kutoka kwa baadhi ya askari
wa Jeshi la Polisi Zanzibar na ombi kwa ajili ya kuwezesha mazungumzo
kati ya Maalim Seif na Mkuu wa Majeshi (CDF), Jenerali Davis
Mwamunyange.
“Baada ya hapo, Rais Kikwete, ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu, amemuagiza
Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu, kuchunguza madai haya
ya CUF na kumletea taarifa. Kadhalika, ametoa maelekezo ofisini kwake ya
kuwezesha mazungumzo kati ya Jenerali Mwamunyange na maafisa wa CUF,”
ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa Rais Kikwete amekuwa akiguswa na hali ya
kisiasa na usalama wa Zanzibar kama ilivyo kwa Watanzania wengine na
amekuwa akifanya kazi bila kuchoka huku akipata ushauri wa kina juu ya
kilichotokea Zanzibar siku chache zilizopita na kupata ufumbuzi.
Taarifa hiyo ilifafanua zaidi kuwa wakati jambo hilo likiwa bado katika
mikono ya ZEC ambacho ni chombo huru cha uchaguzi, Rais Kikwete yuko
tayari kufanya chochote kilicho ndani ya uwezo wake ili kupata suluhisho
jema kuhusiana na hali ya Zanzibar.
Uchaguzi Kufutwa
Suala la kufutwa kwa uchaguzi Zanzibar linadaiwa kuviingiza visiwa hivyo katika mgogoro wa kikatiba na kisheria.
Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, alitaja sababu tisa za kufikia
uamuzi wa kufuta uchaguzi huo kuwa ni pamoja na kura kuongezeka katika
baadhi ya majimbo kisiwani Pemba na pia baadhi ya makamishna wa Zec
kutanguliza itikadi za vyama hadi kuvua mashati ili kupigana.
Kadhalika, alisema katika baadhi ya vituo, masanduku ya kupigia kura
yaliporwa na kwenda kuhesabiwa nje ya vituo, kitendo ambacho ni kinyume
cha sheria ya uchaguzi na pia, kuna taarifa ya kufukuzwa kwa baadhi ya
mawakala wa wagombea na hivyo kushindwa kutekeleza wajibu wao.
Hata hivyo, waangalizi wa ndani na wa kimataifa, wakiwamo Umoja wa Ulaya
(EU), Jumuiya ya Madola Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo ya
Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),
waangalizi wa Marekani na Uingereza, katika ripoti zao wamesema uchaguzi
wa Zanzibar mwaka huu ulikuwa huru na wa haki na kutaka Zec ikamilishe
kazi ya kuhesabu kura na kumtangaza mshindi.
Tagged with: SIASA
Hakuna maoni :