Katika kile kinachoonekana ni kutaka kwenda na kasi ya rais wa awamu ya
tano, Dk. John Magufuli, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Rada kata ya
Majohe, Jimbo la Ukonga, Abdallah Goma, amewatimua ofisini wajumbe
watano wa mtaa na kuwataka waende mitaani kukusanya kero zinazowakabili
wananchi.
Mwenyekiti huyo aliamua kuchukua hatua hiyo baada ya wananchi
kulalamikia tabia ya wajumbe hao kuwadai malipo wakati wanapokwenda
kutaka huduma katika ofisi hiyo, ikiwamo kuandikiwa barua ya utambulisho
benki.
Goma aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na Nipashe jijini Dar es
Salaam jana kutokana na mvutano uliojitokeza kati yake na wajumbe
aliowatimua kugoma kutekeleza agizo lake na kususia vikao.
Alisema baada ya kuapishwa alipanga ratiba ya kila mjumbe kukaa ofisini
kwa muda wa siku mbili, lengo likiwa ni kubaini tabia zao, hivyo katika
kipindi hicho malalamiko ya lugha chafu, kudai malipo ya kuandika barua
ya dhamana na utambulisho yalijitokeza. Tumeamua kutoa huduma bure au
kwa kuchangia gharama kidogo ya uchapishaji lakini siyo lazima ikiwa
mwananchi hawezi kuchangia, alisema. Alisema wajumbe waliruhusiwa
kukaa ofisini kabla ya serikali kuajiri Afisa Mtendaji wa Mtaa, lakini
kwasababu mtendaji ameshaajiriwa kazi ya wajumbe hao ni kukusanya kero
tu.
Mmoja wa wajumbe hao, Siwema Makamba, alisema wao wanajitambua kuwa ni
wajumbe halali waliochaguliwa na wananchi na ni wajibu wao kuwatumikia
kwa nguvu zao zote.
Alisema kitendo cha Mwenyekiti kuwafukuza ofisini ni kuwadhalilisha ili
yeye atumie fursa hiyo kurudisha pesa zake alizotumia kwenye uchaguzi
na kwamba siyo haki kwa wao kwenda kuzunguka mitaani.
Changamoto ya ofisi ymtaa ni kutokuwa na mawasiliano mazuri na
kusababisha mvutano wetu na mwenyekiti, tunapaswa kuondoa tafauti ili
tufanye kazi za wananchi, alisema.
Mmoja wa wakazi wa mtaa wa Rada, Maulid Janga alisema yeye
amesikitishwa na kitendo cha wajumbe kumlipisha Sh. 50,000 kwa ajili ya
kuliinua baraza la mtaa kwenda kushughulikia mgogoro wa mpaka.
Unajua hadi leo mgogoro wa mpaka haujashughulikiwa na pesa zimeliwa
hivi hivi na wajanja, kama walijua hawawezi kutatua tatizo kwanini
wachukue fedha zangu, alisema kwa masikitiko.
Afisa Mtendaji wa kata ya Majohe Serrda Chidaga, alisema yeye
ameshangazwa na mvutano wa wajumbe kungíangíania kukaa ofisini na
kushindwa kwenda mtaani kukusanya kero za wananchi.Baraza la maendeleo
la kata (WDC) limekaa na kujadili suala hilo na kutoa maelekezo kuwa
hawatakiwi kukaa ofisini lakini nashangaa bado wanangíangíania, lazima
hatua za kinidhamu zichukuliwe ikibainika kuna maslahi binafsi,î
alisema.
Tagged with: SIASA
Hakuna maoni :