By Ibrahim Haruna Lipumba
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwamo Zanzibar ilifanya Uchaguzi Mkuu
Oktoba 25, 2015. Kwa upande wa Visiwani, Wazanzibari walipiga kura
kumchagua diwani, mwakilishi, Rais wa Zanzibar, mbunge wa Jamhuri ya
Muungano na Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kutumia Daftari la
Wapigakura la ZEC.
Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) imetumia matokeo ya kura za Rais katika
majimbo ya Zanzibar kujumlisha na matokeo ya majimbo ya Bara na hatimaye
kumtangaza Dk John Magufuli kuwa mshindi wa kiti cha Rais katika
Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano. Kwa uamuzi huo wa kuchukua matokeo
ya majimbo ya Zanzibar yaliyotumia Daftari la Wapigakura la ZEC na
kupiga kura kwenye vituo vilivyoandaliwa na ZEC, Tume ya Uchaguzi ya
Taifa inatambua kuwa uchaguzi uliofanyika Zanzibar chini ya usimamizi wa
ZEC ni halali na matokeo yake ni halali.
Oktoba 28, siku tatu baada ya uchaguzi, Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim
Jecha alitangaza kuwa uchaguzi wa Zanzibar umefutwa. Alipokuwa
anatangaza alikuwa peke yake. Makamu Mwenyekiti hakuwepo. Mkurugenzi wa
ZEC hakuwepo. Wajumbe wengine wa Tume hawakuwepo. Wajumbe wa ZEC
walikuwa Bwawani wakimsubiri Mwenyekiti wao. Walijaribu kuendelea na
kazi ya kuhakiki matokeo chini ya uongozi wa Makamu Mwenyekiti.
Hawakuweza kuendelea na kazi hiyo baada ya Makamu Mwenyekiti kuondolewa
na vyombo vya dola.
Sababu ambazo Mwenyekiti ametoa za kufuta uchaguzi ni pamoja na eti
makamishna wa uchaguzi katika Tume hiyo walidundana kutokana na tofauti
zao. Makamishna walikuwa wanapendelea vyama vyao. Katika vituo vingine,
hasa Pemba, kura zilizopigwa zilikuwa zaidi ya zilizosajiliwa. Masanduku
ya kupigia kura hayakupewa ulinzi wa kutosha na mawakala pamoja na
maofisa wa uchaguzi. Mawakala wa vyama walifukuzwa katika vituo kadhaa.
Vijana walivamia vituo vya kupigia kura wakiwa na lengo la kuzua ghasia
na kadhalika.
Sababu za Mwenyekiti hazina mashiko. Malalamiko haya yalipaswa kutolewa
na mawakala wa vyama mapema. Vituo vya kupigia kura vilikuwa na ulinzi
wa kutosha wa vyombo vya dola. Watazamaji wa ndani na nje walisifia
namna upigaji wa kura Zanzibar ulivyokuwa wa amani na utulivu.
Jecha alieleza kwamba, “Kwa kuzingatia hayo na mengine mengi ambayo
sijayaeleza, Mimi Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar,
nimeridhika kwamba uchaguzi huu haukuwa wa haki na kuna ukiukwaji mkubwa
wa sheria na taratibu za uchaguzi. Hivyo kwa uwezo nilionao natangaza
rasmi uchaguzi huu na matokeo yake yote yamefutwa na kwamba kuna haja ya
kurudia uchaguzi huu.” Mwenyekiti Jecha hakuvitaja vifungu vya Katiba
na sheria vinavyompa mamlaka ya kufuta uchaguzi.
Sura ya tisa ya Katiba ya Zanzibar inaelezea pamoja na mambo mengine
uundwaji, mamlaka na taratibu za uamuzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.
Hakuna kifungu chochote cha Katiba kinachoipa tume au mwenyekiti wake
maamlaka ya kufuta uchaguzi. Katiba inaeleza bayana kuwa uamuzi wa
masuala yote unafanywa na tume kwa pamoja. Kifungu cha 119(10) kinaeleza
kuwa “Kiwango cha mikutano ya Tume ya Uchaguzi ni Mwenyekiti au Makamu
Mwenyekiti na wajumbe wanne na kila uamuzi wa tume ni lazima uungwe
mkono na wajumbe walio wengi.” Mwenyekiti Jecha hakueleza kikao gani cha
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kilichokaa na kufikia uamuzi aliotangaza.
Ukweli ni kwamba Jecha amevunja Katiba ya Zanzibar kwa kutoa uamuzi
mzito bila kufuata taratibu zilizowekwa na Katiba ya Zanzibar. Uamuzi
wake ni batili na hauna nguvu ya kisheria. Katiba na sheria ya Zanzibar
hazijampa mamlaka mwenyekiti na hata tume yote kufuta uchaguzi. Kufanya
hivyo ni kuvunja Katiba ya Zanzibar.
Inaelekea mwenyekiti amepewa shinikizo na ndiyo maana hakuwashirikisha
wajumbe wengine wa ZEC. Bila shaka waliomshinikiza Mwenyekiti wa ZEC
kuvunja Katiba watawashinikiza wajumbe wengine wa ZEC kuunga mkono
uvunjaji wa Katiba uliofanywa na mwenyekiti wao.
Athari za kufuta uchaguzi ni kuleta vurugu za kisiasa na maafa Zanzibar
na Tanzania kwa ujumla. Kwa kuwa matokeo ya kura za Zanzibar kwa
uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano hayaathiri ushindi wa mgombea wa
CCM, matokeo hayo yamekubaliwa. Matokeo ya kura za uchaguzi wa Rais wa
Zanzibar uliofanyika katika mazingira yaleyale na kutumia Daftari la
Wapigakura la ZEC yanakataliwa kwa sababu mgombea wa CCM ameshindwa.
Mwenyekiti wa ZEC ameshinikizwa kufuta uchaguzi wote wa Zanzibar.
Ni wazi wananchi wengi wa Zanzibar hawawezi kukubali kurudia uchaguzi
kwa sababu wenye vyombo vya dola wameamua lazima CCM ishinde ndiyo
matokeo ya uchaguzi yakubaliwe. CCM inawaeleza Wazanzibari mabadiliko ya
Serikali hayawezi kuletwa na vikaratasi vya kura. Mapinduzi daima maana
yake lazima CCM itawale Wazanzibari wakitaka au wasitake. CCM
inawaeleza Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla kama wanataka mabadiliko
aslani hawatayapata kupitia visanduku vya kura. Watafute njia nyingine.
Hili ni jambo la hatari.
Nilidhani CCM imejifunza tangu matukio ya 2001 baada ya uchaguzi wa 2000, uchaguzi wa majimbo 16 ulifutwa na kurudiwa.
CUF ilipotoa taarifa ya kufanya maandamano ya amani nchi nzima kudai
tume huru ya uchaguzi, Katiba Mpya yenye misingi ya demokrasia, utawala
bora na kurudiwa kwa uchaguzi wote wa Zanzibar kama ilivyopendekezwa na
watazamaji wa uchaguzi wa ndani na wa nje, mimi binafsi nilikamatwa
nikapigwa na kuvunjwa mkono na kutupwa jela. Dhahama hiyo iliwakuta
wanachama na viongozi wengine wa CUF. Wananchi wa Zanzibar walipojaribu
kuandamana Januari 27, zaidi ya watu 60 waliuawa na kwa mara ya kwanza
Watanzania zaidi ya 2000 walikimbia nchi yao kwenda Kenya kunusuru
maisha yao. Watanzania tusikubali wanaoishinikiza ZEC kuturudisha huko.
Rais mteule wa Jamhuri ya Muungano, Dk John Magufuli ataapishwa Novemba
5, 2015 na ndiye atakayekuwa Amiri Jeshi Mkuu. Rais Jakaya Kikwete
hatamtendea haki Rais Magufuli kumwachia mgogoro wa Zanzibar ambao
anaweza kuutatua.
Uchaguzi umefanyika Zanzibar na kwa kuzingatia matokeo kwenye vituo
vyote vya wapigakura yaliyotiwa saini na wasimamizi wa vituo na mawakala
wa vyama, mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif
Sharif Hamad ameshinda uchaguzi huo. Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar
ikamilishe uhakiki wa matokeo na kumtangaza mshindi.
Tangu mwaka 1995 sera ya CUF ni kuunda serikali ya umoja wa kitaifa
Zanzibar. Katiba ya Zanzibar ya 2010 imeingiza serikali ya umoja wa
kitaifa kuwa sharti la kikatiba. CCM watakuwa sehemu ya serikali ya
umoja wa kitaifa. Nina uhakika kwa uzalendo wa Kizanzibari wa Maalim
Seif, ataunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayowaunganisha
Wazanzibari.
Propaganda kubwa dhidi ya CUF ni kwamba ikipewa fursa ya kuongoza
Zanzibar, itavunja Muungano. Msimamo rasmi wa CUF ni mfumo wa muungano
wa shirikisho lenye serikali tatu ya Zanzibar, Tanganyika na Muungano
kama uliopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba. Huu ndiyo msimamo wa CUF
tangu mwaka 1995 wakati wa uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi.
Msimamo huu ulifanana na mapendekezo ya Tume ya Jaji Nyalali. CUF
inaheshimu sheria mama ya Jamhuri ya Muungano ambayo ni Makubaliano ya
Muungano.
Tume ya Jaji Warioba ilitoa uhuru kwa Watanzania kutoa maoni kuhusu
Katiba wanayoitaka. Mjadala huu ulitoa mapendekezo mengi likiwamo la
Muungano wa mkataba. Baada ya kuchambua mapendekezo yote, Tume ya Jaji
Warioba iliandaa Rasimu ya Katiba yenye mfumo wa Muungano wa serikali
tatu. Chama cha CUF na Katibu Mkuu wake waliunga mkono mapendekezo ya
Tume ya Jaji Warioba na ndiyo sababu ya kuanzisha Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) katika Bunge Maalumu la Katiba. Wazanzibari wengi
wanaoishi Tanzania Bara wanaunga mkono CUF, lakini pia wanaelewa umuhimu
na faida za Muungano. CUF haitavunja muungano bali itauimarisha kwa
kutumia njia za demokrasia na sheria kutatua kero za Muungano.
Kufuta uchaguzi wa Zanzibar ni kuwanyima Wazanzibari haki ya kuchagua
viongozi wanaowataka. Nikuwaeleza hawawezi kupata mabadiliko kupitia
visanduku vya kura. Watafute njia nyingine. Wanaowanyima Wazanzibari
haki ya kuchagua viongozi wao kwa utaratibu wa kupiga kura ndiyo
wanaoandaa mazingira ya kuvunja Muungano. Rais Kikwete na Rais Ali
Mohammed Shein malizeni tatizo msiliingize taifa kwenye balaa na
kumuachia Rais mteule mgogoro utakaomzuiwa kusimamia ajenda ya maendeleo
ya nchi yetu.
Mwandishi wa makala haya, Profesa Ibrahim Lipumba alikuwa Mwenyekiti wa CUF
Tagged with: SIASA
Hakuna maoni :