Mbunge Mteule wa Jimbo la Kyela, Dkt. Harrison Mwakyembe (pichani)
amesema Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania atatokana
na uteuzi utakaoidhinishwa na Bunge na si taarifa zilizopo sasa katika
mitandao ya kijamii.
Dkt. Mwakyembe ambaye amewahi kuwa Waziri wa Uchukuzi katika Serikali ya
Awamu ya Nne, alisema kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi, Waziri
Mkuu anateuliwa na Rais ambaye huwasilisha jina hilo kwa Spika wa Bunge
na baadaye kupigiwa kura na Wabunge.
Mbunge huyo aliyasema hayo jana Jumapili (Novemba 15, 2015) Mjini
Dodoma wakati alipokuwa akihojiwa na vyombo vya habari kuhusu tetesi
zilizopo katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii
kuhusiana na jina lake kutajwa kuwa ndiye Waziri Mkuu wa Serikali ya
Awamu ya Tano.
“Mimi siwezi kuwasemea wananchi na siwezi
kusema kuna watu wengi wanasema hivi, kwani nafasi ya Uwaziri Mkuu
haiji kwa njia ya kura ya maoni, wala kwa njia ya mitandao ya kijamii
ni nafasi ya uteuzi inayoidhinishwa na bunge na ni mamlaka ya Rais wa
nchi” alisema Dkt. Mwakyembe.
Aidha, Mhe. Mwakyembe aliwataka Watanzania bila kujali itikadi za dini
na vyama vyao wamuombee Rais Dkt. John Pombe Magufuli ili aweze kuchague
viongozi watakao wajibika na ambao wataendana na kasi ya Mhe. Rais.
Wabunge wengine waliotajwa kuwepo kwa uwezekano wa kuteuliwa nafasi ya
Uwaziri Mkuu wa Awamu ya Tano ya Mhe. Rais John Pombe Joseph Magufuli ni
pamoja na Mhe. William Lukuvi, Mhe. Prof. Sospeter Muhongo na Mhe.
January Makamba.
Tagged with: SIASA


Hakuna maoni :