Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea amesema atamfikisha mahakamani
Spika wa Bunge, Job Ndugai kwa kuvunja kanuni baada ya kuwaingiza polisi
ndani ya ukumbi wa chombo hicho.
Polisi hao waliingia ndani ya ukumbi huo wiki iliyopita wakati Rais John Magufuli alipofika kwa ajili ya kuhutubia Bunge.
Kubenea alisema kitendo cha askari kuingia ndani ya Bunge kwa mara ya
mwisho kilitokea nchini Uingereza mwaka 1930 na hakijawahi kutokea tena
isipokuwa nchini.
Alisema kuwa kesi hiyo anatarajia kuifungua Mahakama Kuu wiki ijayo kwa ajili ya kutaka tafsiri ya kanuni hiyo.
Hata hivyo, mkurugenzi wa shughuli za Bunge, John Joel alisema hakuna
kanuni iliyovunjwa kwa askari hao kuingia ndani ya Ukumbi wa Bunge.
Wakati Kubenea akiandaa mpango huo, Kamati ya Wabunge CUF imesema Spika Ndugai ndiye chanzo cha yaliyotokea bungeni.
Ijumaa wiki iliyopita wakati Rais akiingia kutoa hotuba ya kuzindua
Bunge, wabunge hao walipiga kelele wakitaja jina la mgombea urais wa
Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kuonyesha msimamo
wao dhidi ya uamuzi wa kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa visiwa hivyo.
Walipiga kelele hizo wakati Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein akiingia
kwenye ukumbi huo na baadaye wakati Dk Magufuli akiingia ukumbini na
wakagoma kunyamaza hadi walipotakiwa kutoka nje na askari kuitwa ndani.
Wabunge wa upinzani wanadai kuwa Dk Shein si Rais wa Zanzibar, wala
makamu wake wa pili, Balozi Seif Ali Iddi na Spika wa Baraza la
Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho kwa madai kuwa muda wao uliisha Novemba
2, baada ya Uchaguzi Mkuu.
Jana wabunge wa CUF chini ya Mwenyekiti wake, Juma Hamad Omary walitoa
tamko lililokemea na kutoa tahadhari kwa mambo mawili huku wakimtaka
Ndugai kutoyumbishwa na Serikali.
Katibu wa Umoja huo, Hamudu Hassan Bobal alisema vurugu zisingetokea
endapo Bunge hilo lingezingatia tamko la barua ya Ukawa na kusikilizwa
hoja ya mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu aliyeomba
mwongozo akitaka kujua Dk Shein na wenzake wanaingiaje bungeni wakati
madaraka yao yaliisha tangu Novemba 2.
Home
/
SIASA
/
Saed Kubenea Kumburuza Mahakamani Spika wa Bunge Job Ndugai Kwa Kuvunja Kanuni Na Kuwaruhusu Polisi Kuingia Bungeni
Saed Kubenea Kumburuza Mahakamani Spika wa Bunge Job Ndugai Kwa Kuvunja Kanuni Na Kuwaruhusu Polisi Kuingia Bungeni
Tagged with: SIASA
Hakuna maoni :