Beki nyota wa kati wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa, siku kadhaa zilizopita
alivamiwa na watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi na kujaribu kuiba fedha.
Beki huyo,
aliyevamiwa nyumbani kwake Mapambano, Sinza jijini Dar es Salaam, anakumbukwa
kwa kuweka rekodi ya kuwatoa Zamalek katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika
mwaka 2003.
Simba
iliwatoa Zamalek kwa njia ya penalti baada ya mechi ya nyumbani kuwafunga bao
1-0 kabla ya kwenda kurudiana Cairo, Miri na kufungwa bao 1-0 kabla ya kwenda
hatua ya penalti na kuwatoa baada ya Juma Kaseja kupangua penalti kisha
marehemu Christopher Alex kufunga tuta la ushindi.
Pawasa alisema majambazi hao watatu walimvamia saa 11:30
alfajiri nyumbani kwake na kumtaka atoe fedha alizonazo.
Pawasa
alisema, majambazi hao inavyoonekana kama walipewa taarifa za yeye kuwa na
fedha nyingi alizopewa akaweke benki na mmoja wa wafanyabiashara wenzake
aliyemtaja kwa jina moja (linahifadhiwa) siku moja kabla ya tukio hilo.
“Inavyoonekana
kama dili vile limechongwa na watu flani waliokuwa wanajua nina fedha nyingi
nilizotoka nazo ofisini na kurudi nazo nyumbani kwa ajili ya kuzihifadhi.
“Kwa
sababu hao majambazi walipovamia tu nyumbani kitu cha kwanza kuniambia ni
tumefuata fedha zetu, kwa maana ya zile nilizopewa na jamaa yangu ninayefanya
naye biashara, kitu ambacho ni cha kweli lakini tayari nilikuwa nimeshazipeleka
fedha hizo benki.
“Majambazi
hao walikuwa watatu, kati ya hao wawili nilikuwa napambana nao mlangoni
wakitaka kuingia ndani.
“Wakati
napambana na majambazi hao wawili, mmoja alitoa bunduki na kunipiga na kitako
chake na kunipasua usoni, bila kujali nilijaribu kupambana nao hivyohivyo
kuhakikisha ninaokoa uhai wangu.
“Baada ya
kuona nimewashinda walitoka nje na kukimbilia bodaboda waliyokuja nayo
iliyokuwa imeegeshwa nje, mmoja alidondoka, nikafanikiwa kumkamata, muda huo
tayari majirani walikuwa wameshasogea baada ya kusikia makelele.
“Tulivyomkamata
majirani walimshambulia na baadaye kumpeleka kituo cha polisi kabla ya
kupelekwa mahabusu Gereza la Segerea huku wenzake wakitafutwa.
“Baada ya
purukushani hizo kumalizika nilienda Hospitali ya Palestina, Sinza kwa ajili ya
matibabu, nimeshonwa nyuzi tatu ambazo nimetolewa juzi,” alisema Pawasa.
SOURCE: CHAMPIONI
Hakuna maoni :