Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema, kitampa ushirikiano mkubwa, Rais
Dk. John Magufuli, ili aweze kwa ufanisi zaidi mapambano yake dhidi ya
mafisadi na mikakati mingine ya kuinua uchumi wa Watanzania.
Kimesema, kitampa ushirikiano huo Rais Dk. Magufuli, kwa sababu,
aliyoanza kuyafanya na atakayoyafanya baadaye katika uongozi wake wa
Urais anatekeleza yale yaliyomo katika ilani ya Uchaguzi ya CCM ya
2015-2020.
Hayo yalisemwa na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye
alipokuwa akijibu maswali kadhaa yaliyoulizwa na baadhi ya wahariri,
aliokuwa akizungumza nao, katika ziara aliyofanya leo, katika Kampuni ya
New Habari Corporation, Sinza jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wahariri, waliohoji ni kwa nini CCM haijitokezi kumpongeza Dk.
Magufuli katika juhudi ambazo ameanza kuonyesha katika kupambana na
ufisadi ikiwemo kubana fedha za walipa kodi ambazo zingepotea bure
katika masuala yasiyo ya lazima na wakati huohuo kuanza kuwabana
wafanyabiashara wanaodaiwa kukwepa kulipa ushuru.
"Yapo mengi tuliyoanisha katika ilani yetu ya Uchaguzi, na yote
yahahusiana sana na haya mnayoyaona yanafanywa na Rais Dk. John
Magufuli, tena Ilani hii tumeitunga hata kabla ya kumteua kugombea
Urais, Sasa anachofaya ni kuitekeleza ilani hii, isipokuwa mbinu
anazotumia ni ubunifu wake na hili hatuna tatizo nalo kama Chama maana
kiongozi wa aina hii ndiye tuliyemtaka", alisema Nape.
"Najua wapo wanaojaribu kutengeneza magingira ya kumtaka kumtenganisha
Dk. Magufuli na CCM, nawambieni Dk. Magufuli ni zao la CCM na mwana CCM
Kindakindaki, hivyo ni upotoshaji wa hali ya juu kujaribu kuuaminisha
umma kwamba anayofanya Dk. Magufuli hayana uhusiano na maelekezo ya
CCM", aliongeza Nape.
Alisema, baada ya kutengeneza ilani yake, CCM, ilidhamiria kwamba, awamu
hii ya tano ni ya kutafsiri uchumi katika nyanja za huduma za Jamii,
ikiwemo miundomboni, maji, afya na elimu.
"Ni kutokana na lengo hili, ndiyo sababu tukakaa kwa makini na
kuhakikisha ilani hii ya sasa tunamkabidhi mwana CCM ambaye utekelezaji
wake hautakuwa wa mashaka mashaka, Ndiyo huyo Dk. Magufuli, bila shaka
sasa na ninyi ni mashahidi mmeanza kuuona utekelezaji wake wa ilani",
alisema Nape.
Akizungumzia kuhusu Rais Dk. Magufuli kuchelewa kutangaza Baraza lake la
Mawaziri, Nape alisema, Chama Cha Mapinduzi kimeshaunda serikali kwa
kumpata Rais, kilichobaki sasa ni kwa Rais mwenyewe kuteua watendaji
wake, lakini katika kufanya hivyo hakuna mda aliopangiwa kuanza kufanya
hivyo na hashurutishwi na Chama wala sheria.
Nape alisema, Dk. Magufuli hachelewi kuteua Baraza la Mawaziri kwa
sababu anakosa wakuwateua, isipokuwa, anayo namna na mda ambao mwenyewe
Kama Rais amejipangia, na mda huo ukijiri wa kuamua kufanya hivyo
atafanya.
"Tatizo hapa ni kwamba mnayo kiu kubwa ya kutaka kujua nani atawateua,
sasa kiu yenu imepita kiasi, ndiyo maana mnaanza kuhoji, lakini mimi
naamini Dk. Rais Magufuli ataikata kiu yetu, wala msipate taabu ya
kuhoji kila kukicha", alisema Nape.
Nape alisema, mbali na Chama kutengeneza ilani ambayo italeta mageuzi
makubwa ya kiuchumi hapa nchini, pia Watanzania watarajie kuona mageuzi
makubwa ndani ya CCM, kwa sababu yapo njiani kuwadia.
"Kama ilivyo kawaida yetu, kila baada ya uchaguzi mkuu huwa tunafanya
tathmini, baada ya tathmini hiyo, huwa lazima tufanye mageuzi kwa yale
ambayo tumebaini kuwa ni kikwazo kwa uhai na maendeleo ya Chama katika
nyanja mbalimbali, na mageuzi haya tunayafanya kuzingatia mahitaji ya
sasa na wakati ujao", alisema Nape.
Kuhusu Mwenyekiti wa sasa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete kumwachia
Ueneyekiti Rais Dk. Magufuli, Nape alisema, hayo si mambo mageni kwa
CCM, imekuwa ikifanyika katika awamu zote za Urais, hivyo Kikwete
anaweza akaamua kumwachia kabla ya uchaguzi mkuu wa CCM utakaofanyika
mwaka 2017 au kabla ya hapo akiona inafaa.
Zanzibar
Akizungumzia mgogoro wa Zanzibar uliotokana na kufutwa uchaguzi mkuu wa
Rais wa Zanzibar, Nape alikiri kamba ni mbaya na unaitia doa Tanzania,
lakini akasisitiza kwamba njia pekee ya kuumaliza ni kwa mazungumza
baina ya viongozi wa ndani bila kushirikishwa mataifa ya nje.
Alisema, msingi wa mgogoro uliojitokeza Zanzibar, si wa kisheria, bali
ni wa kisiasa zaidi, hivyo juhudi ziwekwe kwenye mazungumzo kuutatua, na
baada ya kuutatua yaendelee kufanyika mazungumzo ambayo yataleta
suluhisho la kudumu kwa kuwa imekuwa ni kawaida kwa Zanzibar kuzuka
migogoro kila baada ya uchaguzi mkuu jambo linaloonyesha kuwa tatizo ni
la asili zaidi kuliko inavyodhaniwa.
Katika mazungumzo yake na wahariri hao wa New Habari Corporation Ltd,
Wachapishaji wa magazeti ya Rais, Mtanzania na Dimba, alivitaka vyombo
vya habari nchini, sasa kushirikiana na Serikali kulijenga taifa.
"Tunajua wakati wa kampeni kulikuwa na mambo mbalimbali ambayo wakati
mwingine vyombo vya habari vililazimika kukampenia vinaowaona kuwa
wanafaa kutokana na sababu mbalimbali, lakini kama tulivyokuwa tukisema,
kwamba baada ya uchaguzi maisha yataendelea, sasa umefika wakati wa
kuendelea na maisha tuwe kitu kimoja", alisema Nape.
Alivitaka vyombo vya habari, kusaidia kuishauri Serikali na CCM, katika
kutekeleza yaliyo bora kwa taifa na hata pale vyombo hivyo vitakapoona
kwamba Chama au serikali vinaenda kinyume, visihofu kukosoa.
Kwa upande wao, Mtariri Mtendaji wa Habari Corporation, Absalom Kibanda
akimpongeza Nape kwa ushirikiano ambao amekuwa akivipa vyombo vya
habari, na kumtaka aendelee kuwacha milango wazi kwa waandishi wa habari
kama ambavyo amekuwa akifanya.
Ziara hiyo ya Nape aliyoianza jana, kwenye vyombo vya habari inatarajiwa
kuendelea kesho kwa kutembelea vyombo vingine vya habari vyenye makao
yake makuu jijini Dar es Salaam
Home
/
SIASA
/
Nape Nnauye Awakata Watu Mdomo Wanaosema CCM Haiungi Mkono Juhudi Anazofanya Rais Magufuli...Asema Haya
Nape Nnauye Awakata Watu Mdomo Wanaosema CCM Haiungi Mkono Juhudi Anazofanya Rais Magufuli...Asema Haya
Tagged with: SIASA
Hakuna maoni :