TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Assalaam alaykum warahmatullahi wabarakaatuhu
Baada ya kumshukuru Mwenye ezi Mungu na Kumtakia rehma na amani kiongozi wetu Bwana Mtume Muhammad S.A.W.
Tunapenda kuwafahamisha ya kwamba baada ya siku chache tutakuwa tumeingia katika Mwezi wa mfungo sita.
Na huu ndio Mwezi aliozaliwa Bwana Mtume S.A.W. kwa mujibu wa kalenda ya kiislamu.
Waislamu wote ulimwenguni unapofika mwezi wa mfungo sita husherehekea juu ya mazazi ya Bwana Mtume S.A.W.
Baraza kuu la Waislamu wa Tanzania
linapenda kuwafahamisha juu ya utaratibu wa matukio tuliyoyapanga katika
kipindi hiki cha mwezi wa kuzaliwa Bwana Mtume S.A.W.
Katika wiki ya kwanza ya mwezi huu wa
mfungo sita kutakuwa na wiki ya misikiti ndani ya wiki hii waislamu
watatakiwa kuongeza nguvu zaidi katika majukumu yao ya kila siku ya
kuhakikisha kuwa mazingira yao yote yanakuwa katika usafi wa hali ya juu
kama ilivyo kawaida.
Vilevile katika mwezi mzima kutakuwa na
mihadhara mbalimbali misikitini, kwenye redio, magazetini pamoja na
televisheni masheikh mbali mbali watashiriki katika mihadhara hii.
Aidha, natoa wito kwa Masheikh na
Maimamu nchi nzima kutumia kipindi hiki cha Shahru Milaad (Mwezi wa
Mazazi ya Mtume S.AW), kumuelezea Mtume (S.a.w) kwa kina katika Nyanja
mbalimbali kama vile elimu, siasa, uchumi, uongozi, utawala bora na
kadhalika.
Pia napenda kuwafahamisha ya kuwa nimeunda timu maalum ambayo nimeipa majukumu ya kufanya maboresho ndani ya BAKWATA.
Timu hii nimeipa pia majukumu ya kupitia
mikataba yote ya BAKWATA ili kuweza kuangalia ile mikataba mibovu na
kuona namna ya kufanya ili BAKWATA iweze kuwa na mikataba yenye maslahi
na Bakwata kwa niaba ya Waislamu.
Aidha timu hii nimeipa majukumu ya kukagua hesabu za BAKWATA kuanzia ngazi ya Makao Makuu na nchi nzima.
Mwisho, kwa mamlaka niliyonayo,
nimemsimamisha kazi Karim Majaliwa - Mkurugenzi wa Utawala wa BAKWATA
Makao Makuu, kwa ajili ya kupisha uchunguzi juu ya kadhia ya magari 82,
pamoja na tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi.
Wabillahi Tawfiiq.
Sheikh Abu bakari Zuberi
Mufti wa Tanzania
05/12/2015
Hakuna maoni :