PLUIJM |
Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm, amegeuka
mbogo na kushusha lawama za wazi kwa benchi la ufundi la timu ya taifa ya
Kilimanjaro Stars, chini ya Abdallah King Kibadeni, kwa kusema kuwa anaua
viwango vya wachezaji wake.
Mdachi huyo akiwa na sura ya hasira, alilalamikia
kitendo cha kipa wake tegemeo, Ally Mustapha ‘Barthez’ kupigwa benchi mwanzo
mwisho kwenye michuano ya Kombe la Chalenji huko Ethiopia, hadi Kili inatupwa
nje ya michuano hiyo kwa kile alichodai ni makosa aliyoyafanya kwenye mchezo na
Algeria.
KIBADENI |
Barthez alilazimika kufanyiwa mabadiliko katika mchezo
wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Algeria, baada ya kuonekana kuwa uchochoro
siku hiyo ambayo Stars ililala mabao 7-0.
Akifafanua kauli yake, Pluijm alisema siku zote kocha
ni sawa na mzazi, hivyo kumpotezea namna hiyo ni kummaliza kabisa kwani
mwishowe atashindwa kujiamini.
“Binafsi sikupendezwa na maamuzi yake. Huku ni kumuua
mchezaji, kumbuka ndiye kipa wangu tegemeo kikosi cha kwanza, yawezekana
hajamtumia akiamini ndiye alikuwa tatizo katika mchezo na Algeria lakini siyo
kweli….siku zote kocha ni sawa na mzazi, sasa unapomnyima chakula unatarajia
nini ndani ya wiki moja zaidi ya kufa?
“Mwisho wa hili ni kukosa ari ya kujiamini
golini ambalo linaweza kuwa tatizo kwetu,” alifunguka Mdachi huyo.
Katika michuano ya Chalenji, Barthez amepigwa benchi
katika mechi zote nne, huku kinda wa Azam, Aishi Manula akianza katika mechi
tatu za makundi na Saidi Mohammed ‘Duda’ wa Mtibwa Sugar akikaa langoni katika
mchezo wa robo fainali dhidi ya Ethiopia ambao tulitupwa nje.
SOURCE: CHAMPIONI
Hakuna maoni :