Katibu
Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Mwesigwa Selestine
kesho Jumatano anatarajiwa kuongozana na mshambuliaji wa timu ya Taifa
ya Tanzania na klabu ya TP Mazembe ya Congo DR, Mbwana Samatta kuelekea
nchini Nigeria kwenye sherehe za utoaji wa tuzo kwa wachezaji bora
barania Afrika.
Mwesigwa anatarajiwa kuondoka na Samatta kuelekea Nigeria katika
mji wa Abuja ambapo sherehe za utoaji tuzo hizo zitafayika Alhamisi
Januari 7, ambapo siku ya sherehe hizo Katibu Mkuu ataambatana na Ofisa
ubalozi wa Tanzania nchini Nigeria.
Mbwana Samatta anawania tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa
wachezaji wa ndani, huku pia akiwa mfungaji bora wa michuano ya Ligi ya
Mabingwa (CAF CL) baada ya kuifungia klabu yake ya TP Mazembe mabao 8 na
kuibuka mabingwa wapya wa michuano hiyo.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi
amemtakia kila la kheri Mbwana Samatta katika kinyanganyiro hicho cha
uchezaji bora na kusema kwa niaba ya watanzania wote wanamuombea dua
njema aweze kuibuka mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani.
Samatta anawania tuzo ya mchezaji bora wa Afrika pamoja na mlinda
mlango wa TP Mazembe, Robert Kidiaba (Congo DR) na mshambuliaji wa
Etoile du Sahel Baghdad Boundjah (Algeria).
IMETOLEWA NA TFF
Hakuna maoni :