Mwanasheria mkuu wa Chadema ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki,
Tundu Lissu ametofautisha kilichomkuta Edward Lowassa kwenye sakata la
Richmond na kilichomkuta Profesa Sospeter Muhongo kwenye sakata la
Escrow bungeni.
Akiongea katika kipindi cha Mada moto cha Channel Ten, Lissu alieleza
kuwa kwa kutumia ripoti za kamati za bunge zilizomhukumu Lowassa mwaka
2008 na ripoti za kamati ya bunge ilizomhukumu Profesa Muhongo mwaka
2014/2015 kuna utofauti mkubwa.
Alisema kuwa ripoti ya Mwakyembe ilieleza kuwa Lowassa anawajibika kwa
makosa ya watu watano wa chini yake ambao aliwataja majina na kwamba
hakuna sehemu ilimtaja Lowassa kuhusika moja kwa moja na sakata la
Richmond.
Alisema kuwa kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyokuwa chini
ya Zitto Kabwe na Deo Filikunjombe, ilieleza wazi kuwa Profesa Muhongo
alishiriki kudanganya kuwa fedha zile hazikuwa za umma na baadaye
ikabainishwa na kamati hiyo kuwa zilikuwa fedha za umma.
“Kwa mujibu wa kamati ya Mwakyembe, Lowassa aliwajibika kwa sababu ya
makosa ya hawa watu… Sasa hayo ni ya Lowassa. Yanalingana kiasi gani na
ya Profesa Muhongo, yanalingana kiasi gani na ya Profesa Muhongo
aliyesema kuwa bilioni 300 na ushee zilizotolewa Benki Kuu zikagawanywa
kama njugu ni hela binafsi.
“CAG akachunguza akasema kuna hela za Umma, Takukuru wakachunguza
hawajatuletea taarifa bungeni mpaka leo. Bunge likachunguza likasema
hizi ni fedha za umma na hawa watu wawajibike na wakawajibishwa. Kuna
ulingano gani hapo? Na hapo nazungumzia taarifa za kamati hizi mbili za
bunge,” alisema Lissu.
Alikosoa uteuzi wa Profesa Muhongo akidai kuwa Bunge liliazimia
kumfukuza na leo serikali inamrudisha kama vile hakuna kilichotokea hata
kabla mwaka mmoja haujapita.
Udaku Special Blog
Tagged with: SIASA
Hakuna maoni :