Wakati
Simba ikiwa kwenye moto wake, ghafla kumeibuka taarifa ya kutakiwa kwa
kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Mwinyi Kazimoto na timu ya Al Markhiya
ya Qatar aliyokuwa akiitumikia awali.
Taarifa
zinaeleza kuwa hii ni mara ya pili sasa tangu kuanza kwa msimu wa
2015/16 Waarabu hao wanajaribu kuleta ofa hiyo juu ya mchezaji huyo
baada ya uongozi wa Simba kuikataa ile ya awali iliyokuja mwanzoni mwa
msimu huu.
Kazimoto
alitimkia Al Markhiya kwa mara ya kwanza mwaka 2012 akitokea Simba SC
kabla ya kurejea nchini mwaka jana ikielezwa kuwa ameachwa na timu hiyo
kutokana na sheria mpya za shirikisho la nchi hiyo kupunguza idadi ya
wachezaji wa kigeni.
Hata
hivyo, baada ya tathmini ya mechi zake, benchi la ufundi la timu hiyo
limegundua kuwa viungo wapya walioko katika kikosi hicho hawakidhi kama
ilivyokuwa kwa Kazimoto, hivyo wamewasilisha tena ombi lao wakitaka
Simba iwasikilize.
“Ndiyo,
wale jamaa wa Markhiya wanamtaka tena Mwinyi kwa kigezo kuwa uwezo wake
ulikuwa mkubwa zaidi ya viungo waliopo hapo kwa sasa, hii ni mara ya
pili kuleta ombi hilo tangu kuanza kwa msimu huu, mara ya kwanza
walimtaka tukawagomea lakini sasa wamerudi tena,” alisema moja ya
wajumbe wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo.
Alipotafutwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe kulitolea
ufafanuzi suala hilo, alisema: “Hizo taarifa kama zipo basi hazijafika
kwangu, siwezi kusema lolote kuhusu Kazimoto mpaka nipate hizo taarifa
na itahitajika makubaliano ya wote kabla ya kuamua kumuuza au la.”
Hakuna maoni :