Hii
ni habari njema kwa wachezaji na wadau wa soka la Bongo baada ya
taasisi inayojulikana kwa jina la Enlightened Football Foundation (EFF)
kuweka wazi jinsi wanavyoweza kuwasaidia wachezaji, makocha na hata
mameneja jinsi ya kurahisisha mambo na kupata mafanikio kupitia mchezo
huo.
Kwa
miaka ya hivi karibuni ingawa soka limeonekana kukua kwa maana ya
ushabiki lakini wahusika wanaonekana kunyonywa na kushindwa kuhimili
maisha, taasisi hiyo imekuja na mifumo mbadala ambayo imedokeza michache
kati ya mingi waliyonayo katika kuhakikisha wanatumia nafasi waliyonayo
kuliinua soka la Bongo.
Mtendaji
Mkuu wa EFF, Daniel Mwakasungula ameliambia gazeti hili kuwa taasisi
hiyo ambayo ilisajiliwa rasmi Novemba 11, 2015, inajishughulisha katika
kurekebisha vipengele vya mikataba, kuwatengeneza vijana wachanga kukua
katika msingi ya soka, namna ya kukusanya pesa nje ya mshahara wao
kupitia vipaji vyao na mengine mengi.
“Ofisi
zetu zipo pale Kinondoni Kwa Manyanya na kwa kifupi tupo kwa ajili ya
kuendeleza soka nje ya uwanja kwa kutoa elimu, kuelekeza baadhi ya mambo
ambayo ni vikwazo kwa wachezaji, makocha au mameneja, haya yote
yanafanyika bure.
“Tuna
mawakili pale ambao watawaelimisha na kupitia mikataba ya wachezaji au
makocha kabla ya kutia saini, lakini kumjuza na kumwelewesha kijana juu
ya kazi yake, nini afanye, ajitunze vipi ili afikie malengo na pia kuwa
na umuhimu wa mameneja wanaofahamu kazi zao na mengine mengi,” alisema
Mwakasungula.

Hakuna maoni :