Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF) limetangaza kuwa Machi 20, mwaka huu ndiyo siku
ya kutolea uamuzi juu ya hatma ya timu itakayopanda daraja kucheza Ligi
Kuu Bara msimu ujao kutoka Kundi C.
Timu
za Polisi Tabora na Geita Gold Sports ndizo zinasubiri hatma hiyo baada
ya kumaliza mechi zake zote zikiwa na pointi 30, huku TFF ikiwa na
mashaka juu ya matokeo ya mwisho ya mechi zao ambapo Geita iliifunga JKT
Kanembwa mabao 8-0, huku Polisi Tabora ikiikandamiza JKT Oljoro mabao
7-0 na kudai kwamba kuna mchezo mchafu wa upangaji matokeo ulifanyika,
kitendo ambacho hakikubaliki kwenye soka.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Rais wa TFF, Jamal Malinzi, amesema kutokana na
uzito wa ishu hiyo, walilazimika kuipeleka kesi hiyo katika kamati ya
nidhamu ya shirikisho hilo ili kutoa hukumu kwa haki na usawa.
“Najua
wengi wanataka kufahamu ni lini utapatikana mustakabali wa timu
iliyopanda daraja kutoka Kundi C, niwaambie tu kesi hiyo itasikilizwa
Machi 20, mwaka huu baada ya kufika kwenye kamati ya nidhamu ambayo
ndiyo wenye jukumu la kusimamia ishu hiyo nzima.
“Kulikuwa
kuna kila dalili za upangwaji matokeo na hukumu ya aliyetenda kosa hilo
iko wazi, kama si kifungo cha maisha cha soka basi ni timu inashushwa
daraja, lakini kutokana na kanuni za mashindano za Ligi Daraja la Kwanza
kutokuwa na kipengele kinachotoa adhabu hizo, ndiyo maana tukaihamishia
katika kamati ya nidhamu, baada ya hukumu kutolewa na kama upande mmoja
hautaridhika basi unaruhusiwa kukata rufaa,” alisema Malinzi.
Malinzi
aliongeza kuwa, hawakuweza kutoa hukumu mapema kutokana na uzito wa
jambo hilo lililohitaji uchunguzi wa kina kwani kutokana na mchezo wa
soka kuwa ni ‘fair play’, kuna uwezekano kwa timu zote zilicheza ‘fair
play’ na kufungwa kihalali, ndiyo maana wanasubiri uchunguzi ufanyike
kwanza kabla ya yote.
Hakuna maoni :