Jose Mourinho hajui lolote kuhusu yeye kuwa Meneja wa Manchester United lakini anatarajia kurejea kama Meneja kwa ajili ya Msimu ujao.
Mapema Mwezi huu, habari zilivuja kuwa Mourinho ndie atatwaa wadhifa huko Old Trafford baada ya Mkataba wa Meneja wa sasa Louis van Gaal kukatishwa.
Mourinho, mwenye Miaka 53, aliondolewa Chelsea Mwezi Desemba ikiwa ni Miezi 7 tu tangu aipe Klabu hiyo Ubingwa wa England.
Alipoulizwa ikiwa atambadili Louis van Gaal huko Old Trafford, Mourinho alisema: “Hilo ni Swali la Dola Milioni 1!”
Mourinho aliongeza: “Hakuna Mtu anaejua na mimi ndio wa kwanza kutojua. Nasoma vitu tofauti vingi sana.”
Huku pia akihusishwa na kurejea Klabu alizowahi kuziongoza huko nyuma, Inter Milan ya Italy na Real Madrid ya Spain, Mourinho alieleza: “Kuanza Msimu mpya ujao na Klabu mpya na Mradi mpya ndio kitu bora kwangu.”
Hivi sasa kila kukicha hatima ya Van Gaal, mwenye Miaka 64, ndio kitu kinachonadiwa sana licha ya kwamba Mkataba wake na Man United unakwisha mwishoni mwa Msimu ujao wa 2016/17.
Hivi sasa Man United wapo Nafasi ya 5 kwenye Ligi Kuu England wakiwa Pointi 6 nyuma ya Timu ya 4 lakini wametinga Robo Fainali ya FA CUP na Alhamisi wanapambana na Klabu ya Denmark, FC Midtjylland, wakitakiwa kupindua kipigo cha 2-1 cha Wiki iliyopita ili wasonge.
Hakuna maoni :