Shahidi wa tatu wa mlalamikaji, James
Lembeli katika kesi ya kupinga matokeo ya ubunge yaliyompa ushindi
Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Jumanne Kishimba (CCM) jana alitinga
Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga akiwa na mzigo wa masufuria, akidai
alipewa kwa ajili ya kumpigia mgombea ubunge wa CCM.
Mbele ya Jaji Moses Mzuna anayesikiliza
shauri hilo, Cesilia Gregory wa Nyahanga mjini Kahama alikiri kupokea
zawadi ya masufuria hayo kutoka kwa Wakala wa Kishimba ili ampigie
kura.
Gregory alidai Oktoba 19, 2015, Kikundi
cha Amani waliitwa nyumbani kwa Hamad Hilal na kumkuta Ezra Machogu,
ambaye alikuwa ni Wakala wa Kishimba akigawa masufuria yalitolewa kwa
ajili ya kumuombea kura mgombea ubunge wa CCM.
Hata hivyo, kulitokea mvutano baada ya
Wakili wa Kishimba, Antony Nansimire kumtaka shahidi kuwataja
wanakikundi 20 ambao walipewa masufuria hayo, hivyo kuwataja 22 na
kwamba ongezeko hilo lilisababishwa na baadhi ya wanaume waliojiunga
kuhamasisha utafutaji wapiga kura wa Kishimba.
Wakati huohuo, mawakili wa mdai katika
shauri la kupinga matokeo ya ubunge Jimbo la Kyerwa mkoani Kagera,
Benedicto Mutungirehi wamejitoa.
Hatua hiyo ilifuatia makosa ya kisheria
yaliyobainishwa katika hati ya kiapo cha shahidi wa pili, Pastory
Bagambila ambaye tayari alikuwa mbele ya Mahakama kutoa ushahidi wake.
Baada ya kubaini makosa hayo, Wakili
Erasto aliiomba Mahakama kumuondoa shahidi huyo kutoka kwenye orodha ya
mashahidi kabla ya kutoa ombi la kujadiliana kwa muda na mteja wake.
Hata shahidi wa tatu, Alistides Boniface
alipoitwa naye hati yake ya kiapo ilibainika kuwa na kasoro za
kisheria, hali iliyomtia hofu Wakili Erasto kuwa yawezekana viapo vya
mashahidi wote 36 vilivyowasilishwa vina kasoro.
Kabla ya kujitoa, wakili Erasto
alimuomba Jaji Maisario Munisi anayesikiliza shauri hilo, kuahirisha kwa
muda ili wajadiliane na mteja wao.
Waliporejea mahakamani baada ya dakika
30, Wakili Erasto alimweleza Jaji Munisi kuwa wanaomba kujitoa kwa
maelekezo ya mteja wao.
Kutokana na hali hiyo, Mutungirehi
aliiomba Mahakama kumpa muda kutafuta wakili, ombi lililokubaliwa na
Jaji Munisi na kuiahirisha hadi Machi 22.
Mbunge wa sasa wa jimbo hilo kupitia CCM, Innocent Bilakwate anawakilishwa na Wakili Peter Matete.
Baadhi ya maombi yake ya msingi,
Mutungurehi anadai kulikuwapo na ukiukwaji sheria, taratibu na kanuni
katika kuhesabu kura na kudai kulitawaliwa na usiri bila kumhusisha.
Hakuna maoni :