Siri
ya Simba kufanya vizuri mfululizo katika mechi zake za Ligi Kuu Bara
hivi karibuni imefichuka baada ya ushindi wa juzi Jumamosi ilioupata
mkoani Tanga ilipopambana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Siri
hiyo si nyingine bali ni uamuzi wa uongozi wa Simba kupitia kwa rais
wake, Evans Aveva ulioufanya hivi karibuni baada ya kuamua kumteua
aliyewahi kuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Mzee Hassan Dalali kuwa mshauri
mkuu wa benchi la ufundi la timu hiyo.
Dalali
alikabidhiwa jukumu hilo kwa siri na uongozi huo baada ya mwenendo
mbaya wa timu hiyo katika mechi zake za awali za ligi kuu.
Habari
za kuaminika kutoka ndani ya Simba zimedai kuwa, tangu Dalali
alipokabidhiwa timu hiyo, imeshinda zaidi ya mechi 12 na imepoteza moja
tu dhidi ya Yanga ambapo ilifungwa kwa mabao 2-0.
“Hali
hiyo imewafanya viongozi wetu kuwa na matumaini makubwa kuwa safari hii
tunaweza kuwa mabingwa wa ligi kuu kwa sababu Dalali amefanikiwa kwa
kiasi kikubwa kulituliza benchi letu la ufundi lakini pia viongozi
kutomwingilia kocha katika kazi yake.
“Ukiachana
na hilo pia Dalali anaijua vizuri ligi kuu kwani katika kipindi chake
Simba ilikuwa ikifanya vizuri, hivyo atatusaidia kukabiliana na
ujanjaujanja wote ambao umekuwa ukifanywa kwa ajili ya kuimaliza timu
yetu,” kilisema chanzo hicho cha habari.
Alipoulizwa
kuhusiana na hilo, Dalali alisema: “Ni kweli kabisa hivi sasa
nimekabidhiwa timu na uongozi na ninavyoongea na wewe mida hii nipo
katika basi na timu tunatoka Tanga.
“Tangu nikabidhiwe jukumu hilo ni muda mrefu kidogo kama mechi kumi na kitu hivi zilizopita, hata hivyo kuhusiana na mambo mengine yanayohusu timu sasa siwezi kuyazungumzia, naomba unisamehe kwa hilo.”
Hakuna maoni :