Ingawa haijajulikana rasmi nini kilichomo ndani yake, baadhi ya watu waliohojiwa wanatarajia CAG kubaini mchwa wanaotafuna fedha za umma na namna ya kukabiliana nao.
Aidha wengine wanatarajia taarifa ya hali bora zaidi ya usimamizi wa fedha za umma kuliko kipindi cha nyuma.
Ripoti hiyo awali ilikuwa imepangwa kuwasilishwa bungeni mwishoni mwa wiki (Aprili 22) kabla ya kuahirishwa hadi leo.
“Ni kweli CAG atawasilisha ripoti kesho (leo) bungeni, ”Naibu Katibu wa Bunge na Utawala, Joel Joel alithibitisha juu ya kuwasilishwa kwa ripoti hiyo leo.
Miongoni mwa wabunge waliozungumza na mwandishi wa habari hizi, wamesema wanatarajia CAG kuonesha mambo mazuri kwa maana ya taasisi zilizofanya vizuri katika usimamizi wa fedha za umma lakini pia mambo mabaya.
“Lazima ripoti itaibua madudu maana walizoea (watendaji serikali) kana kwamba hapakuwapo na serikali,” alisema Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy na kusisitiza kuwa pamoja na wabunge wenzake, watamsaidia Rais John Magufuli kupambana na ubadhirifu serikalini.
Keisy alisema akiwa mbunge, anaamini pamoja na wenzake, wanachosubiri ni kuona ripoti hiyo na kuhakikisha wanaohusika na kuchezea fedha za serikali, kabla ya kufikishwa mahakamani, wanarudisha fedha hizo.
“Atakachosema CAG sisi tutakuwa tayari kusimama kusaidia Rais aendelee kupambana na ubadhirifu,” alisema.
Kwa upande wake, Mbunge wa Mbinga Vijijini, Martin Msuha, alisema ripoti hiyo ni muhimu katika usimamizi wa serikali na inategemewa kuwa na mambo mazuri na mabaya kwa maana ya majipu ambayo yatapaswa kutumbuliwa.
Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza alisema matarajio waliyo nayo ni kwamba ubadhirifu na wizi utakaoibuliwa na ripoti hiyo utashughulikiwa mara moja.
“Kama kuna ubadhirifu, mishahara hewa na wizi vyote vishughulikiwe...kama kuna ubadhirifu na wizi wowote, mwizi mahali pake ni jela,” alisema Rweikiza akishutumu uwapo wafanyakazi hewa katika halmashauri yake.
Hakuna maoni :