Baada ya shirika la umeme nchini kuzima mitambo ya kuzalisha umeme
katika kituo chake cha Mtera, kituo kingine cha kuzalisha umeme cha
Kidatu kinachotegemea maji kutoka Bwawa la Mtera kinatarajiwa kuzima
mitambo yake hivi karibuni kutokana na kuishiwa maji kwa ajili ya
kuendesha mitambo hiyo.
Meneja wa Tanesco kituo cha kuzalisha umeme cha Kidatu mhandisi Justus
Mtolela amesema kituo hicho chenye uwezo wa kuzalisha megawati 200
kimepunguza uzalishaji wake hadi kufikia megawati 30.
Amesema hali hiyo inatokana na
kukosekana kwa maji ya kuendeshea mitambo ambapo kina cha maji katika
bwawa la Kidatu kimeshuka kutoka mita za ujazo 450 hadi kufikia mita 441
huku kiwango cha mwisho kinachoruhusiwa kuzalisha umeme kikiwa ni mita
433.
Kukauka kwa maji katika bwawa la Mtera na Kidatu ni athari inayotokana
na kukauka kwa maji ya mto Ruaha mkuu ambao ndiyo tegemeo la bwawa hilo
la Mtera linalohudumia pia bwawa la Kidatu kwa pamoja na mto Lukosi na
Iyovi ambayo na yenyewe imekauka.
Hivi karibuni baadhi ya wataalamu na wadau wa rasilimali za maji
wamekuwa na maoni na mapendekezo kwa serikali juu ya hatua zinazopaswa
kuchukuliwa ili kunusuru rasilimali hiyo na kuifanya kuwa endelevu ikiwa
ni pamoja na kutazama upya mgawanyo wa maji kwa sekta mbalimbali na pia
kusimamia ufanisi katika matumizi yake.
Hakuna maoni :