Na Saleh Ally
SAKATA la beki
Said Juma Nyosso limekuwa maarufu hata kuliko matokeo ya mechi ya watani, Simba
na Yanga iliyochezwa jijini Dar es Salaam, Jumamosi.
Nyosso alimtomasa
makalio nahodha wa Azam FC, John Bocco, baada ya kuwa wamejibizana na Bocco
akarusha mguu kumpiga teke, alipomkosa, Nyosso akatumia mwanya huo kufanya
alichotaka.
Tayari Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF), limetangaza adhabu ambayo hakika ni kali, maana miaka
miwili bila kucheza soka na faini ya Sh milioni mbili, si adhabu ndogo.
Wapo ambao
wanaona adhabu hiyo inatosha, wapo wanaoona ni ndogo, wanataka Nyosso afungiwe
maisha lakini wapo pia wanaoona Nyosso ameonewa, wanataka ipunguzwe. Maoni,
kila mtu ana yake, kikubwa ni kuangalia kanuni.
Watu wengi
wameonekana kuchukizwa na tukio hilo maradufu kwa kuwa Nyosso amerudia. Aliwahi
kufanya hivyo kwa Elius Maguli, mwanzoni mwa mwaka huu, nakumbuka ilikuwa
Januari.
Mwisho akaomba
radhi, akasisitiza kwamba ameidhalilisha familia yake, ya Maguli, pia ya Mbeya
City. Hata mwaka haujapita, karudia tena baada ya kuwa amekumbana na adhabu ya
kufungiwa mechi nane.
Mjadala ni mpana,
lakini jana nimeona viongozi wa Mbeya City pamoja na Kocha Juma Mwambusi kila
mmoja akitoa maoni yake wakati akilizungumzia suala hilo.
Wamezungumzia
suala la kuunda kamati, suala la kusubiri mkanda wa video kwamba kama Nyosso
atakuwa amefanya watamchukulia hatua, kama hakufanya watakata rufaa.
Mwambusi
amekaririwa akisema ameuona mkanda wa video Nyosso hajafanya lolote! Nyosso
mwenyewe, amesema hakumbuki kumfanyia hivyo Bocco na watu wanamhukumu kutokana
na mazoea. Maana yake alichokifanya huko nyuma!
Hakika
inashangaza sana, kila mmoja anajua namna Nyosso alivyo muhimu sana katika
kikosi cha Mbeya City. kwa alichokifanya si suala la kujaribu kukwepesha au
kutaka kuonyesha mnamjali kwa kutaka kupotosha mambo.
Suala la kusema
TFF wamekurupuka, hoja nyingine zimezuka mbona fulani hakuadhibiwa, sawa. Kuna
haki ya kuhoji, lakini adhabu aliyopewa Nyosso ni sahihi iwe fundisho hasa kwa
wale wanaotenda maovu, wanaidanganya jamii kwa kuomba radhi halafu wanafanya
tena. Haya ni maovu kujumlisha dharau.
Kumtetea Nyosso
kweli ni haki ya viongozi wa Mbeya City, lakini si wakati huu na mnapaswa kuwa
makini sana kuingiza vichekesho (comedy) katika suala hili. Acheni watu wa
mtaani wataniane halafu nyie fanyeni kazi kuhakikisha mnalikomesha kabisa.
Video zipo lundo,
hazidanganyi, hazifichi na hakuna haja ya kulazimisha eti Nyosso anaonewa. Eti
kuna watu walitengeneza picha ili Nyosso aadhibiwe, vichekesho vya namna hii ni
propaganda za kisiasa ndani ya mchezo wa soka.
Mwacheni Nyosso
atumikie au apate anachostahili kutokana na upuuzi aliouanzisha kwa mikono yake
mwenyewe. Mbeya City itakuwa haina cha kulaumiwa kama itatenda haki kwa kuwa
viongozi wakumbuke, siku nyingine atatendwa mchezaji wao, halafu watashindwa
hata kuinua midomo kulalamika kwa kuwa leo wanaingia kwenye njia ya kusifia
maovu.
Hakuna haja ya
kuzungusha, Nyosso amefanya ujinga na ameharibu heshima ya Mbeya City ambayo
sasa bado ni changa sana. Huu ndiyo msimu wa tatu Ligi Kuu Bara. Lazima
viongozi wanaonyesha timu hiyo ni ya Wanambeya, inahudumiwa na fedha za
wananchi pia wadhamini.
Hawa wote
wanapaswa kuombwa radhi, wanapaswa kuona haki inatendeka na suala la nidhamu
ndiyo msingi linapewa kipaumbele.
Ninaamini
viongozi wa Mbeya City hawatakubali kuuingia mkenge wa kuwa watetezi wa Nyosso
kwa maana ya kwamba hakufanya lolote. Kama wana hoja ya ziada, wanaweza kuiinua
lakini sasa, kilicho mezani ni Nyosso amefanya ujinga, tena akiwa na kitambaa
cha unahodha cha Mbeya City.
Hakuna maoni :