SIASA

SIASA

MAONI

MAONI

BURUDANI

MICHEZO

/ / MBEYA CITY, MSITAKE KULIFANYA SUALA LA NYOSSO KAMA SEHEMU YA UTANI






Na Saleh Ally

SAKATA la beki Said Juma Nyosso limekuwa maarufu hata kuliko matokeo ya mechi ya watani, Simba na Yanga iliyochezwa jijini Dar es Salaam, Jumamosi.



Nyosso alimtomasa makalio nahodha wa Azam FC, John Bocco, baada ya kuwa wamejibizana na Bocco akarusha mguu kumpiga teke, alipomkosa, Nyosso akatumia mwanya huo kufanya alichotaka.



Tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limetangaza adhabu ambayo hakika ni kali, maana miaka miwili bila kucheza soka na faini ya Sh milioni mbili, si adhabu ndogo.



Wapo ambao wanaona adhabu hiyo inatosha, wapo wanaoona ni ndogo, wanataka Nyosso afungiwe maisha lakini wapo pia wanaoona Nyosso ameonewa, wanataka ipunguzwe. Maoni, kila mtu ana yake, kikubwa ni kuangalia kanuni.



Watu wengi wameonekana kuchukizwa na tukio hilo maradufu kwa kuwa Nyosso amerudia. Aliwahi kufanya hivyo kwa Elius Maguli, mwanzoni mwa mwaka huu, nakumbuka ilikuwa Januari.



Mwisho akaomba radhi, akasisitiza kwamba ameidhalilisha familia yake, ya Maguli, pia ya Mbeya City. Hata mwaka haujapita, karudia tena baada ya kuwa amekumbana na adhabu ya kufungiwa mechi nane.



Mjadala ni mpana, lakini jana nimeona viongozi wa Mbeya City pamoja na Kocha Juma Mwambusi kila mmoja akitoa maoni yake wakati akilizungumzia suala hilo.

Wamezungumzia suala la kuunda kamati, suala la kusubiri mkanda wa video kwamba kama Nyosso atakuwa amefanya watamchukulia hatua, kama hakufanya watakata rufaa.



Mwambusi amekaririwa akisema ameuona mkanda wa video Nyosso hajafanya lolote! Nyosso mwenyewe, amesema hakumbuki kumfanyia hivyo Bocco na watu wanamhukumu kutokana na mazoea. Maana yake alichokifanya huko nyuma!



Hakika inashangaza sana, kila mmoja anajua namna Nyosso alivyo muhimu sana katika kikosi cha Mbeya City. kwa alichokifanya si suala la kujaribu kukwepesha au kutaka kuonyesha mnamjali kwa kutaka kupotosha mambo.



Suala la kusema TFF wamekurupuka, hoja nyingine zimezuka mbona fulani hakuadhibiwa, sawa. Kuna haki ya kuhoji, lakini adhabu aliyopewa Nyosso ni sahihi iwe fundisho hasa kwa wale wanaotenda maovu, wanaidanganya jamii kwa kuomba radhi halafu wanafanya tena. Haya ni maovu kujumlisha dharau.



Kumtetea Nyosso kweli ni haki ya viongozi wa Mbeya City, lakini si wakati huu na mnapaswa kuwa makini sana kuingiza vichekesho (comedy) katika suala hili. Acheni watu wa mtaani wataniane halafu nyie fanyeni kazi kuhakikisha mnalikomesha kabisa.



Video zipo lundo, hazidanganyi, hazifichi na hakuna haja ya kulazimisha eti Nyosso anaonewa. Eti kuna watu walitengeneza picha ili Nyosso aadhibiwe, vichekesho vya namna hii ni propaganda za kisiasa ndani ya mchezo wa soka.



Mwacheni Nyosso atumikie au apate anachostahili kutokana na upuuzi aliouanzisha kwa mikono yake mwenyewe. Mbeya City itakuwa haina cha kulaumiwa kama itatenda haki kwa kuwa viongozi wakumbuke, siku nyingine atatendwa mchezaji wao, halafu watashindwa hata kuinua midomo kulalamika kwa kuwa leo wanaingia kwenye njia ya kusifia maovu.



Hakuna haja ya kuzungusha, Nyosso amefanya ujinga na ameharibu heshima ya Mbeya City ambayo sasa bado ni changa sana. Huu ndiyo msimu wa tatu Ligi Kuu Bara. Lazima viongozi wanaonyesha timu hiyo ni ya Wanambeya, inahudumiwa na fedha za wananchi pia wadhamini.



Hawa wote wanapaswa kuombwa radhi, wanapaswa kuona haki inatendeka na suala la nidhamu ndiyo msingi linapewa kipaumbele.



Ninaamini viongozi wa Mbeya City hawatakubali kuuingia mkenge wa kuwa watetezi wa Nyosso kwa maana ya kwamba hakufanya lolote. Kama wana hoja ya ziada, wanaweza kuiinua lakini sasa, kilicho mezani ni Nyosso amefanya ujinga, tena akiwa na kitambaa cha unahodha cha Mbeya City.


Hii ni mara ya pili ndani ya mwaka mmoja, adhabu haikwepeki kama kweli klabu inataka kuwaonyesha watu inaamini nidhamu ndiyo msingi wa mafanikio.

«
Next

Chapisho Jipya

»
Previous

Taarifa za zamani

About Unknown

Asante kwa kutembelea SELASINI HABARI,NITAKUHABARISHA, KUKUELIMISHA NA KUKUBURUDISHA HIVYO USIKOSE KUTEMBELEA SELASINIHABARI.BLOGSPOT.COM.

Hakuna maoni :

Leave a Reply