MAPENZI yanatingisha dunia! Ndivyo unavyoweza kusema kufuatia nyota
wawili wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Omary Nyembo
‘Ommy Dimpoz’ kuzinguana laivu nchini Marekani, Risasi Jumamosi
limevujishiwa na lina mchapo kamili.
Chanzo makini kilichoshuhudia sakata hilo lililotokea hivi karibuni
nchini Marekani kulipokuwa na hafla ya utoaji wa tuzo za Afrimma ambapo
Diamond alitwaa 3 huku Dimpoz akipata 1, kimenyetisha kuwa, wawili hao
walizinguana wakiwa wanataka kuingia kwenye ukumbi ulioandaliwa kwa
ajili ya utoaji wa tuzo hizo.
“Walipokuwa wanaingia ukumbini, Dimpoz akakutana na Diamond sasa Diamond
akataka kumsalimia ndipo Dimpoz akachomoa na kumpa maneno ya kejeli
ambayo yalimkasirisha nusu wazichape.
“Kila mtu alijua jamaa watashikana mashati. Lakini sema ile busara ya
haraka iliwajia, hawakufikia hatua hiyo mbaya,” kilisema chanzo.
CHANZO CHA BIFU
Kikaendelea: “Unajua Dimpoz alikataa kupokea salamu ya Diamond maana
anasema ni mnafiki. Anadai kwamba, Diamond anapokuwa na watu anajifanya
hana tatizo na Dimpoz lakini akiwa na marafiki wa Dimpoz huwa
anamzungumzia vibaya na wakikutana na Dimpoz anamsalimia kinafiki ndiyo
maana mwenzake akamaindi.”
WEMA ATAJWA
Kikizidi kulipambanua bifu la mafahari hao wawili, chanzo hicho kilidai
kuwa, sababu kubwa ya bifu hilo ilianza muda mrefu baada ya Diamond
kumhisi Dimpoz anatembea na Wema Sepetu ‘Madam’ ambaye alikuwa mpenzi
wake kwa muda mrefu kisha akamwagwa.
“Kumbe Diamond ana kinyongo na mwenzake. Alimwagwa na Wema lakini
nafikiri bado moyoni anampenda sana. Sasa alipoona siku chache baada ya
kuachana, ghafla mrembo huyo akaonekana katika pozi tata na Dimpoz,
akamuwekea bifu pasipo hata kumuuliza kama ni kweli au la,” kilisema
chanzo na kuongeza:
“Tangu hapo, Diamond amekuwa akimsema vibaya Dimpoz kupitia marafiki
zake kitu ambacho Dimpoz anakiona ni unafiki kwani hamwambii mwenyewe.
Huwezi amini kule Marekani, Diamond alikuwa ndiye aliyetangulia kufika
lakini badala ampokee mwenzake ambaye ni mgeni, akampotezea halafu
ukumbini akajifanya anamsalimia.”
WABONGO WAWASHANGAA
Chanzo hicho kilizidi kumwaga ubuyu kuwa, kitendo cha wawili hao
kuzinguana ukumbini wakati wanatokea sehemu moja kiliwashangaza Wabongo
waishio nchini humo ambao walikwenda kushuhudia utoaji wa tuzo hizo
kwani walitegemea wawili hao wangekuwa kitu kimoja.
“Wabongo wenzao waishio Marekani waliwashangaa sana. Hawajui kwamba huku
ndiyo walitakiwa kuonesha umoja wao. Kwanza ndiyo wanainuka katika tuzo
kubwa halafu wao wanaleta za uswahilini, itawagharimu siku moja,”
kilisema chanzo hicho.
DIMPOZ AFUNGUKA
Baada ya kupenyezewa ubuyu huo, mwanahabari wetu alianza kumtafuta
Dimpoz ili aweze kutoa ufafanuzi juu ya kile kilichotokea ambapo
alipopatikana, alifunguka:
“Daah! Nani kawapa hizo habari? Nyinyi kweli mnajua kunusa. Ni kweli tulipishana na jamaa (Diamond) kule Marekani.
“Lakini si unajua tena… pengine Diamond ana kinyongo chake na mimi
sipendi mtu anayeishi kwa vinyongo, ndiyo maana nilikataa salamu yake,
yakatokea hayo lakini kimsingi namshukuru Mungu hatukukunjana wala
nini.”
DIAMOND SASA
Jitihada za kumpata Diamond ili aweze kueleza kwa upande wake hazikuzaa
matunda kufuatia kuwepo kwa taarifa kuwa alikuwa safarini nje ya nchi.
“Jamaa siyo rahisi kumpata sababu yupo safarini nje ya nchi labda
umcheki tena baadaye,” alisema mtu wa karibu na Diamond pasipo kutaja
msanii huyo ameelekea wapi.
TUJIKUMBUSHE
Baada ya Diamond kumwagwa na Wema mwishoni mwa mwaka jana, baadaye
Februari mwaka huu, picha zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii
zikimwonesha Dimpoz na Wema wakiwa kitandani, hotelini nchini Afrika
Kusini ‘Sauz’.
Baadhi ya vyombo vya habari nchini viliandika kuwa wawili hao wana
uhusiano wa kimapenzi huku ikielezwa kwamba, uhusiano huo ulikuwepo kwa
siri hata wakati Wema akiwa na Diamond.
Hata hivyo, baadaye ikaja kuelezwa kuwa, Wema na Dimpoz walikuwa nchini
humo wakitengeneza video ya wimbo wa Dimpoz uitwao Wanjera.
Tagged with: BURUDANI
Hakuna maoni :