SIASA

SIASA

MAONI

MAONI

BURUDANI

MICHEZO

/ / Dr. Magufuli Ashauriwa Kutofanya Uteuzi Wa Baraza la Mawaziri Kwa Kulipa FADHILA



RAIS Mteule wa awamu ya tano katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.John Pombe Magufuli, ameshauriwa kuwa makini katika uundaji wa Baraza lake la Mawaziri kwa kuepuka masuala ya kujuana au kuteua kwa shinikizo la baadhi ya wanasiasa wenye masilahi binafsi.

Akizungumza na m,wandishi wetu jana jijini Dar es Salaam, Mhadhiri mstaafu wa masuala ya Uongozi katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Morogoro Dkt. Alfred Chimage, alisema tatizo kubwa la viongozi wa Tanzania ni kutokuwa na uwezo wa kutambua watu wanaofaa, wanaopaswa kuwateua ili kuwasaidia kuongoza nchi.

Aliongeza kwamba viongozi wengi waliofanikiwa ni wale wenye uwezo mkubwa wa kupanga timu sahihi ya wasaidizi katika masuala ya uongozi.

Dkt. Chimage alisema Dkt. Magufuli anaweza kuwa kiongozi mzuri lakini hofu iliyopo anaonekana kuzungukwa na kundi kubwa la wanasiasa hususan wanaoamini kwamba wametoa mchango mkubwa kwake kumfikisha hapo alipo; hivyo kutaka kupata fadhila za nafasi za juu za uongozi kwa ajili ya ndugu zao wa karibu na hata watoto wao.

"Inawezekana Magufuli ni kiongozi mzuri, lakini ukiangalia anavyoonekana ni kama tayari amemezwa na baadhi ya wanasiasa wanaojinasibu na kujiona kana kwamba amefikia hatua hiyo kwa nguvu yao.

"Mbali na hilo, ukiangalia mazingira ya siasa zinazomzunguka ni kama kwamba kuna kundi la wanasiasa wakongwe ndani ya CCM linaloamini kwamba litaendelea kumpa maelekezo kwa hatua mbalimbali ikiwemo ya kuteua baraza la mawaziri.

"Akinaswa kwenye mtego huo atakuwa amefanya kosa kubwa la kwanza kwenye uongozi wake," alisema mtaalamu huyo na kuongeza;

"Kuna wanasiasa wengi ambao unawaona moja kwa moja wanajisogeza kwa nguvu sana kwa Magufuli si kwa kumsaidia kuongoza nchi peke yake, bali wana malengo maalumu kuhakikisha wananufaika kwenye uongozi wake kwa ndugu, jamaa na hata watoto wao kupewa madaraka ya juu".

Alisema katika kipindi hiki, Dkt. Magufuli anapaswa kuwa makini zaidi ili kuepusha Serikali yake kupoteza imani mbele ya Watanzania kwa kuendekeza kile kinachofahamika kama siasa za kujuana na kubebana kama njia ya kulipa fadhila.

Alisema Dkt. Magufuli anapaswa kutambua kwamba yeye ni rais wa Watanzania wote na si rais wala rafiki ya familia au kundi fulani la watu, hivyo anapaswa kuteua mawaziri na watendaji wengine kwa kigezo cha uwezo.

 
"Magufuli asipokuwa makini malalamiko ya kwanza ya wananchi yatakuja baada tu ya kutangaza Baraza lake la Mawaziri, kama litaonekana kubeba watu kwa misingi ya kujuana. Anachopaswa kufanya ni kuacha mamlaka husika zifanye proper vetting (Uhakiki wa kina) wa sifa za kila anayeona anafaa".

"Asiteue baraza kwa misingi ya huyu ni rafiki yangu au ni ndugu au mtoto wa mtu fulani, hapana atajiharibia kabisa," alisema.

Ameshauri pia kuwa makini kuepuka watendaji wote ambao kwa njia moja ama nyingine walihusishwa na kashfa mbalimbali kwenye serikali iliyopita.
"Wakati wa kampeni Magufuli ameimba sana neno mabadiliko, mabadiliko haya yasiwe ya kusema tu. Wananchi wanasubiri waone mabadiliko hayo kuanzia timu ya watu atakaowateua kufanya nao kazi. Watu wanatarajia kuona mawaziri safi wasio na 'makandokando'.

"Anapaswa kuwa makini na kila mtu. Atumie ile falsafa ya mke wa Kaisari. Aachane na wote waliosemwa vibaya kwenye serikali iliyopita hata kama wanaonekana kuchapa kazi. Mifano ipo mingi, waliochafuka kwa Escrow, kwa uozo wa bandari, ununuzi wa mabehewa mabovu. Ili aingie kama kiongozi safi na mtu wa mabadiliko ya kweli azibe mapema mianya kama hii. Watanzania watapata imani na atafanikiwa," alisema.

Alisisitiza kwamba Magufuli anapaswa kuwa makini kuepuka mitego ya kindugu, urafiki na kifamilia ambayo alisema imeonekana kuwa tatizo kubwa katika masuala ya uongozi hapa nchini.

Alisema kigezo pekee cha mtu kuteuliwa kuwa waziri au kiongozi wa nafasi yoyote ile ni kuchapa kazi.

«
Next

Chapisho Jipya

»
Previous

Taarifa za zamani

About Unknown

Asante kwa kutembelea SELASINI HABARI,NITAKUHABARISHA, KUKUELIMISHA NA KUKUBURUDISHA HIVYO USIKOSE KUTEMBELEA SELASINIHABARI.BLOGSPOT.COM.

Hakuna maoni :

Leave a Reply