Azam FC inaendesha mambo yake kama timu za
Ulaya hasa England, kwani baada ya kukataa straika wake Didier Kavumbagu
kujiunga na Simba kwa mkopo, imemruhusu nyota huyo kwenda Sweden.
Mtu wa karibu na Kavumbagu amesema straika huyo
raia wa Burundi amepata timu Sweden na Azam imekubali kuondoka kwake na sasa
inatafuta mbadala wake klabuni.
Kocha wa Azam, Stewart Hall, alikataa Kavumbagu
kujiunga na Simba kwa mkopo kwa kile kilichodaiwa kutotaka kujiongezea timu
pinzani katika ligi huku akionekana kuruhusu mchezaji huyo kujiunga na Yanga.
Kavumbagu anaonekana hana furaha ndani ya Azam
kutokana na kutokuwa na uhakika wa nafasi kikosi cha kwanza, sasa anakwenda
Sweden alipo straika wa zamani wa Simba, Emmanuel Okwi.
Hall amesema kuwa: “Imekuja
ofa hapa Kavumbagu anatakiwa na timu moja ya Sweden yeye pamoja na Farid Mussa
na Mudathir Yahya, hatuna jinsi sasa tunatafuta mbadala wa Kavumbagu.”
Hata hivyo, Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba
alipotafutwa alisema: “Bado ofa hiyo haijafika kwangu, ila kama imekuja
nitaiona tu na labda niseme hatuna pingamizi kwa Kavumbagu kama anataka
kuondoka, muhimu ni makubaliano tu.”
Hakuna maoni :