Aliyekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa amesema
awamu ya pili ya safari yake ya kuelekea Ikulu ndio kwanza imeanza na
kuwataka watu wote wanaomuunga mkono kutokata tamaa.
Lowassa, ambaye ameshika nafasi ya pili katika mbio za urais wa Jamhuri
ya Muungano akiweka rekodi ya kukusanya kura milioni 6.07 ambayo ni
rekodi kwa mgombea wa upinzani, alitoa kauli hiyo jana mchana katika
hafla ya chakula cha mchana ya kuishukuru timu yake ya kampeni
iliyofanyika Kawe, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wakuu wa
vyama vinavyounda Ukawa, wanahabari na familia yake.
“Nimefarijika sana, asanteni kwa msaada mlionipa, sina cha kuwalipa,”
alisema waziri huyo mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne
aliyeihama CCM na kujiunga na Chadema mwezi Julai.
“Ukweli ni kwamba kila mmoja alifanya kazi yake. Tujiandae kwa awamu ya pili na safari ndiyo imeanza,” alisema na kushangiliwa.
“Unaweza kuchelewesha bahati ya mtu, lakini hauwezi kuiondoa,” aliongeza.
Hata hivyo, Lowassa hakueleza awamu ya pili itahusisha mambo gani.
Tangu kumalizika kwa uchaguzi huo, Lowassa amezungumza na vyombo vya
habari mara mbili, mara ya mwisho akieleza jinsi alivyowasilisha
pingamizi lenye hoja tatu kuhusu mwenendo wa uchaguzi kwa mwenyekiti wa
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva ambalo liligonga
mwamba.
Katika tamko lake, Lowassa alikuwa akipinga matokeo ya kura za urais
yaliyokuwa yakitangazwa na NEC akidai kuwa si halisi na kuitaka isitishe
kutangaza, lakini tume hiyo haikueleza lolote na badala yake iliendelea
kutangaza matokeo ya majimbo na baadaye mshindi wa urais.
Mambo hayo matatu yaliyowasilishwa NEC ni kupunguzwa kwa kura zake,
kuongezewa kura kwa mgombea wa CCM na kutangazwa matokeo batili kwa
wagombea wa Ukawa.
Lowassa aliyeanza kwa kuwatambulisha watu wake wa karibu waliomshauri
masuala muhimu na nyeti katika kampeni, akiwemo waziri wa zamani wa
Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, alizungumza kwa kifupi, akitoa mfano wa
jinsi majeshi ya ukombozi wa nchi mbalimbali barani Afrika yalivyorudi
nyuma kujipanga baada ya kushindwa.
Muda mfupi kabla ya Lowassa kueleza hayo, mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe aliufananisha Uchaguzi Mkuu na vita, akisema kulikuwa na njama za
makusudi za kuhakikisha Lowassa hapati ushindi.
Alisema wagombea ubunge kutoka vyama vinavyounda Ukawa vya NCCR-Mageuzi,
Chadema, NLD na CUF, waliibiwa kura na ushindi kupewa wagombea wa CCM.
Mbowe alisema kwa kuwa hawawezi kupinga matokeo ya urais mahakamani, watafungua kesi za kupinga matokeo ya ubunge.
“Tunachofanya, tunarudi nyuma, tunajipanga kukata rufaa kupinga matokeo katika majimbo zaidi ya 30,” alisema Mbowe.
“Wagombea wetu waliokuwa wabishi na kupigana kwelikweli walitangazwa
washindi, lakini kuna majimbo ambayo wagombea wetu waliporwa ushindi
waziwazi kabisa. Kwa kuwa ubunge unapingwa mahakamani tutafanya hivyo,”
alisema Mbowe.
Miongoni mwa majimbo ambayo matokeo yake yalikuwa na ubishi ni
Nyamagana, ambako mbunge maarufu wa Chadema, Ezekiah Wenje alishindwa na
mgombea wa CCM,Stanslaus Mabula baada ya mvutano uliochukua muda mrefu.
Pia mbunge wa NCCR Mageuzi, David Kafulila wa Kigoma Kusini aliangushwa
baada ya matokeo kuibua mzozo mkali uliosababisha polisi kuingilia
kati.
Mbowe pia alisema kuwa wanahamishia nguvu Zanzibar kuungana na mgombea
urais kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad kudai haki yake.
Mbowe alisema kitendo cha kufutwa kwa uchaguzi huo kina mkanganyiko
mkubwa na kusisitiza kuwa kuanzia wiki ijayo Ukawa itapiga kambi kwenye
visiwa hivyo kuhakikisha haki inatendeka.
Baadhi ya viongozi wa Ukawa waliohudhuria hafla hiyo ni makamu
mwenyekiti wa Chadema –Bara, Profesa Abdallah Safari, mwenyekiti wa NCCR
na mbunge mteule wa Vunjo, James Mbatia na kaimu katibu Mkuu wa
Chadema, Salum Mwalimu.
Source:Mwananchi
Tagged with: SIASA
Hakuna maoni :