Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif
Sharif Hamad, amesema CUF inaendelea kutafuta haki ya Wazanzibar ya
kutaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) kuendelea kutangaza matokeo ya
uchaguzi ili mshindi ajulikane na hatimaye kuapishwa.
Aliyasema hayo wakati akizungumza na wafuasi wa chama hicho katika makao
makuu ya CUF Mtendeni juzi, baada ya kurudi safari yake ya kuonana na
rais wa awamu ya nne, Dk. Jakaya Kikwete, Ikulu, jijini Dar es Salaam.
Aliwaambia wanachama hao kuwa hakuna kurudi nyuma katika kudai haki yao
kwa njia ya amani na utulivu ili matokeo yatangazwe na mshindi wa urais
ajulikane.
“Niwahakikishieni vijana na wanachama wa CUF kuwa hakuna kurudi nyuma,
tunaendelea kudai haki yetu na tunashukuru dunia nzima inatuunga mkono
kwa hili,”alisema Maalim Seif, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK).
Alisema kuwa wapinzani wao, Chama Cha Mapinduzi (CCM) mpango wao ni
kutaka kuendelea kuwa katika madaraka wakijua kuwa muda wa Dk. Ali
Mohammed Shein wa kukaa madarakani umekwisha, lakini wanang’ang’ania
aendelee kinyume cha Katiba.
Aidha, alisema kuwa hakuna dawa yoyote ya kumaliza mgogoro ulipo
Zanzibar isipokuwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) kuendelea kutoa
matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu ili mshindi ajulikane na
kuapishwa.
“Wanaosema kuwa uchaguzi urejewe waachieni wenyewe, sisi katika CUF
hakuna msamiati huo kwa sasa kurejea uchaguzi, huo ndio msimamo wetu,”
alisisitiza Maalim Seif.
Alisema kuwa kwa uwezo wa Mungu haki yao wataipata na kuwataka vijana
kuendelea kuwa watulivu na kuendelea kutunza amani ya nchi kwa
kutokubali kuchokozeka. Alisema CUF na viongozi wake hawatakubali kuwa
chanzo cha kuvuruga amani ya nchi na wataendelea kuhubiri amani wakati
wote.
Mvutano wa kisiasa unaoendelea Zanzibar ulisababishwa na Mwenyekiti wa
Zec, Jecha Salim Jecha, kutangaza kufuta uchaguzi wa Zanzibar wa rais na
wawakilishi Oktoba 28, kwa madai kuwa ilibaini kuwapo kwa kasoro kadhaa
kisiwani Pemba.
Hata hivyo, waangalizi wa nje na ndani wameeleza kushangazwa ha hatua ya
Jecha, kwa kuwa hawakushuhudia kasoro zozote hadi walipotoa ripoti ya
awali.
Aidha, asasi za nchini na mataifa kadhaa yakiwamo Uingereza, Ireland na
Marekani yameshatoa taarifa ya kushangazwa na uamuzi wa Jecha na
kushauri mchakato wa kutangaza matokeo uendelee.
MTOTO WA KARUME AIBUA MAPYA
Mjadala kuhusiana na hatma ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofutwa na
Jecha, umechukua sura mpya, baada ya mmoja wa watoto wa Rais wa zamani,
Dk. Amani Abeid Karume, kuibuka na kufichua kile anachoamini kuwa ni
sababu ya utata uliojitokeza sasa.
Mtoto huyo ni Mwanasheria, Fatma Karume, ambaye akiwa pamoja na Rais wa
Chama cha Wanasheria wa Zanzibar (ZLS), Awadh Ali Said, waliuambia umma
kupitia mahojiano ya moja kwa moja kwenye kituo kimoja cha televisheni
jijini Dar es Salaam juzi kuwa sababu mojawapo ya kufutwa kwa uchaguzi
wa Zanzibar ni muundo wa uongozi unaomruhusu rais wa visiwa hivyo kuwa
mmoja wa wajumbe katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Akifafanua, Fatma alisema kuwapo kwa nafasi ya moja kwa moja ya Rais wa
Zanzibar kwenye Baraza la Mawaziri kunaibua mgongano inapotokea mshindi
wa upande mmoja akiwa ni wa kutoka chama kingine na hiyo ni sababu
mojawapo wanayoamini kuwa imechangia kufutwa kwa uchaguzi na pia kukwaza
ukuaji wa demokrasia visiwani humo.
Alisema ni dhahiri hali huwa ngumu kwa baraza la mawaziri linaloundwa na
watu wa itikadi ya chama kimoja kuchanganyika na mwingine mwenye
itikadi tofauti, hasa katika mazingira ya kuwa na usiri katika baadhi ya
mambo na kwamba, hilo huchangia kusuasua kwa maendeleo ya kidemokrasia
visiwani Zanzibar.
Hata hivyo, ili kuondokana na mgogoro kama uliopo sasa, Fatma alisema ni
muhimu kwa viongozi wa kisiasa nchini na kwingineko barani Afrika
kuzingatia sheria na katiba zilizopo.
Awali, ilisisitizwa na wanasheria hao kuwa uamuzi wa kufutwa kwa
uchaguzi wa Zanzibar uliochukuliwa na Mwenyekiti wa Zec peke yake,
haukuzingatia sheria na katiba na ndiyo maana sasa kumeibuka mgogoro wa
kikatiba kwani kifungu kinachotumika kuhalalisha hoja ya kuendelea
kubaki madarakani kwa Dk. Shein kimekuwa kikitafsiriwa vibaya kwa
maslahi ya kisiasa.
Akielezea zaidi, Awadh alisema hakuna kifungu chochote kinachomruhusu
Jecha kufuta uchaguzi na ndiyo maana hadi sasa hakuna mtu aliyethubutu
kutaja kwa uwazi ni sheria ipi imempa nguvu mwenyekiti huyo wa Zec
kufuta uchaguzi wa Zanzibar.
Source: Nipashe
Tagged with: SIASA
Hakuna maoni :