Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC) wa Marekani umeonya kuwa hali ya
kisiasa Zanzibar na tukio la hivi karibuni la watu kukamatwa chini ya
sheria mpya ya uhalifu mtandaoni yanaweza kuathiri vigezo vya kuiwezesha
Tanzania kupata msaada.
Katika barua ya MCC ya Novemba 19, ambayo imesainiwa na Naibu Makamu wa
Rais wa Idara ya Operesheni ya Miradi kwa Afrika, Jonathan O. Bloom
kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile,
mfuko huo umetaka maelezo kuhusu utatuzi wa mgogoro wa Zanzibar pamoja
na ufafanuzi wa sheria ya uhalifu wa mtandaoni.
“MCC inashukuru kwa uongozi na dhamira yako wakati wa mchakato mzima wa
maendeleo ya mradi huu. Msaada wa dola milioni 472 (ambazo ni zaidi ya
Sh trilioni moja), una nafasi kubwa ya kusaidia kuleta mageuzi katika
sekta ya nishati na kuwaunganisha maelfu ya watu katika gridi.
“Lakini mgogoro wa Zanzibar na ukamataji watu wa hivi karibuni kupitia sheria mpya ya uhalifu mtandaoni umetutia wasiwasi.
“Kama ujuavyo, mataifa washirika wa MCC wanapaswa kuendeleza na
kuonyesha dhamira ya utawala bora, ambayo ni pamoja na kufuata misingi
ya demokrasia na kulinda uhuru wa kutoa mawazo.
"Hata hivyo, matukio ya karibuni yanaifanya MCC na wadau wetu kujawa na
maswali kuhusu dhamira hiyo,” inasomeka barua hiyo ya MCC iliyosainiwa
na Bloom.
Kwa mujibu wa barua hiyo, MCC inafuatilia kwa karibu nyendo za Serikali
katika ushughulikiaji wa masuala hayo ya utawala bora, hasa kipindi hiki
kuelekea mkutano wa mwezi ujao wa bodi ya mfuko huo.
“Utatuzi wa mgogoro wa Zanzibar kwa namna ya kuridhisha pande zote
husika na haja ya kuiona Serikali ikifafanua hadharani nia yake na
sheria ya uhalifu wa mtandaoni, kama vile kuchapisha utekelezaji wa
kanuni zinazoakisi mchango wa mdau na kuonyesha dhamira ya kuendelea
kulinda uhuru wa kutoa maoni, kutaisaidia MCC kuitathimini Tanzania kwa
namna chanya juu ya kuendelea kwa dhamira yake ya kutimiza sharti la
kufuzu kupata misaada,” ilisema barua hiyo.
Barua hiyo ilimalizia kwa kusema: “Wasiwasi huu ni kikwazo cha mipango
yetu ya ushirika. Tunaamini utashughulikia wasiwasi huu ipasavyo na
tunatarajia kupata jibu kutoka kwako.”
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Likwelile, hakupatikana na hata alipotafutwa kwa njia ya simu hakupokea.
Pamoja na juhudi hizo, pia alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu hakujibu,
ambapo alipotafutwa Msemaji wa Wizara ya Fedha, Ingiahedi Mduma, kuhusu
barua hiyo ya MCC, alisema hana taarifa na hajaiona.
“Sina taarifa na wala sijaiona barua hiyo, hivyo siwezi kusema chochote
labda mpaka nitakapoongea na bosi aniambie kama amepokea barua hiyo,”
alisema Mduma.
Mwanzoni mwa Oktoba mwaka huu, Rais mstaafu Jakaya Kikwete akiwa nchini
Marekani kuhudhuria shughuli za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN),
alikutana na Mtendaji Mkuu wa MCC, Dana J. Hyde na watumishi waandamizi,
akiwamo Makamu wa Rais wa Operesheni za mfuko huo, Kamran Khan.
Katika mkutano huo, MCC ilitangaza kuwa Tanzania imetimiza masharti yote
ya kupatiwa awamu ya pili ya fedha za maendeleo kutoka katika mfuko
huo, kuanzia mwakani, zaidi ya dola za Marekani milioni 472.8, sawa na
zaidi ya Sh trilioni moja za Tanzania.
Katika mkutano huo, Rais mstaafu Kikwete, aliambatana na ujumbe wa
maofisa kadhaa akiwamo Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Yusuf Omar Mzee.
Katika awamu ya kwanza ya fedha za MCC, Tanzania ilipata dola za Marekani milioni 698 (sawa na Sh trilioni 1.46).
Kama MCC wataridhika na maelezo ya Serikali kupitia Wizara ya Fedha,
Tanzania itakuwa imepata jumla ya Sh trilioni 2.45 kwa awamu zote mbili
kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika kipindi cha miaka 10.
Awamu ya kwanza ya fedha hizo zilitumika kujenga Barabara za Tunduma- Sumbawanga, Tanga-Horohoro na Namtumbo- Songea- Mbinga.
Desemba 10, mwaka jana, Marekani pia ilibainisha hatua ya uamuzi wa
utolewaji wa fedha za awamu ya pili za MCC utategemea hatua
zitakazochukuliwa na Serikali kuhusu sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh
bilioni 200 katika akaunti ya Tegeta Escrow.
Uamuzi huo wa Marekani ambayo inafadhili miradi mingi ya mabilioni ya
fedha nchini, ulionekana kama mtihani wa pili kwa Rais mstaafu Kikwete,
baada ya ule wa maazimio ya Bunge yaliyotaka viongozi wakiwamo mawaziri
waliotajwa katika kashfa hiyo kuwajibishwa.
Waliowajibishwa na Rais Kikwete ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa, Sospeter Muhongo na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Wengine ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini,
Eliakimu Maswi na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick
Werema.
Chanzo: Mtanzania
Home
/
MATUKIO
/
Marekani Yaipa Kibano Tanzania .....Yaitaka Serikali itoe Maelezo Uchaguzi Zanzibar na Sheria ya Mtandao , Yatishia kusitisha Msaada wa Trilioni
Marekani Yaipa Kibano Tanzania .....Yaitaka Serikali itoe Maelezo Uchaguzi Zanzibar na Sheria ya Mtandao , Yatishia kusitisha Msaada wa Trilioni
Tagged with: MATUKIO
Hakuna maoni :