KAMPUNI ya Said Salim Bakhresa (SSB) inachunguzwa na vyombo vya dola kwa
tuhuma za kushiriki kukwepa kodi na hivyo kuikosesha serikali mabilioni
ya fedha kutokana na makontena yaliyohifadhiwa kwenye bandari yake ya
nchi kavu (ICD) ‘kupotea’ bila kulipiwa kodi.
Tayari Mamlaka ya Mapato (TRA) imepiga marufuku SSB kuingiza makontena
katika bandari hiyo kavu ambako ndiko kunadaiwa kufanyika kwa vitendo
hivyo vya ukwepaji wa kodi kutokana na baadhi ya makontena kupotea
katika mazingira ya kutatanisha.
Katika barua iliyoandikwa kwenda kwa Meneja Mkuu wa SSB iliyosainiwa na
Wolfgang Salia kwa niaba ya Kamishna wa Ushuru na Forodha wa TRA,
inaeleza kuwa usitishwaji huo unatokana na kampuni hiyo ya Bakhresa
kuchunguzwa kwa tuhuma za kuwepo madai ya kujihusisha na ukwepaji wa
kodi kwa baadhi ya kontena zilizoingia na kutoka kwenye ICD yake.
Kwa mujibu wa barua hiyo, vitendo hivyo vya ukwepaji wa kodi vimefanywa
kinyume cha Sheria ya Ushuru wa Pamoja wa Nchi za Jumuiya ya Afrika
Mashariki ya Mwaka 2004 na hivyo kuikosesha Serikali mapato.
“Unafahamu kwamba uondoaji wa bidhaa kutoka eneo linalodhibitiwa na
forodha, ambalo kodi na ushuru wa serikali haujalipwa ni kinyume na
sheria kwa mujibu wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Usimamizi
wa Forodha ya mwaka 2004 na kanuni zake kwa vile husababisha upotevu wa
mapato ya Serikali.
“Kwa sababu hiyo, imeamuriwa kukuzuia kupeleka makontena katika bandari
yako kavu kuanzia tarehe ya barua hii, hadi suala hili litakapotatuliwa.
Pande zote zinazohusika zinapaswa kutii amri hii.
“Kutokana na sababu hizo, tunasimamisha upelekaji wa makontena katika
bandari yako kavu. Usitishaji unaanza mara moja. Hata hivyo utoaji wa
bidhaa zilizopo katika bandari hiyo tajwa utaendelea,” ilisema sehemu ya
barua hiyo iliyoandikwa Novemba 17, mwaka huu.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Walipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Richard Kayombo alipoulizwa juu ya suala hilo jana,
alikiri kampuni hiyo kuchunguzwa, lakini akagoma kuzungumzia kwa undani
kwa kuwa suala hilo liko kwenye uchunguzi.
“Mimi siwezi kulizungumzia suala hilo kwa sababu liko kwenye uchunguzi
na wanaofanya uchunguzi huo ni state organ (vyombo vya dola). Katika
hatua hiyo, mimi siruhusiwi kusema lolote,” alisema Kayombo.
Meneja wa Kundi la Makampuni ya Said Salim Bakhresa, Said Mohamed
alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, alisema yeye hahusiki na masuala ya
ICD badala yake mambo hayo aulizwe Meneja wa ICD aliyemtaja kwa jina
moja la Khan. “Mimi niulizie unga umekosekana... Sihusiki kabisa na
mambo hayo,” alisema Mohamed.
Hata hiyo, Mohamed aligoma kutoa mawasiliano ya Khan, akisema: “Hiyo
namba mimi hapa sina, wewe mtafute tu huko ICD atakupa maelekezo zaidi.”
Habari zilizopatikana jana pia zilieleza kuwa mmoja wa wafanyakazi wa
SSB anayeishi maeneo ya Kinyerezi (jina tunalihifadhi), alivamiwa na
kundi la maofisa wa Serikali kuanzia asubuhi hadi jioni na kufanya
upekuzi kwake.
“Tangu asubuhi hawa jamaa wamekuja hapa wakamchukua mjumbe wa eneo hili
na kwenda naye kufanya upekuzi, hadi sasa hivi wanaendelea kufanya kazi
hiyo,” alisema Tito Bagule, mkazi wa eneo hilo.
Tayari Rais John Magufuli ameshamsimamisha Kamishna Mkuu wa TRA, Rished
Bade kutokana na tuhuma za uzembe na rushwa na kusababisha upotevu wa
makontena zaidi ya 349 yenye thamani ya Sh bilioni 80.
Upotevu huo umegundulika baada ya makontena hayo kuonekana kwenye mifumo
ya Mamlaka ya Bandari, lakini haimo kwenye mifumo ya TRA.
Kabla ya kusimamishwa kazi, Bade alikiri kupotea kwa makontena hayo,
wizi ambao alisema unafanywa kati ya bandari kuu na bandari kavu (ICD)
ya Ubungo.
Alisema kutokana na upotevu wa kontena hizo mmiliki wa bandari hiyo
ameamriwa kulipa faini ya Sh bilioni 12.6 na hadi sasa alishalipa Sh
bilioni 2.4.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI),
Diwani Athuman, amesema tayari jeshi hilo limeanza upelelezi kuhusu
kashfa ya upotevu wa makontena iliyobainishwa hivi karibuni na
kusababisha baadhi ya vigogo wa TRA kusimamishwa kazi.
Pamoja na upelelezi huo, alisema wameanza uchunguzi wa mali za
wafanyakazi wote waliohusishwa na kashfa mbalimbali TRA kama
ilivyoagizwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ili kubaini kama zinaendana
na kipato chao halisi.
Akizungumza na mwandishi wetu jana, Diwani alikiri kuwa jeshi hilo
linawashikilia watumishi wanne kati ya watano wa TRA ambao jeshi hilo
liliagizwa liwakamate na kuwahoji kuhusu sakata la upotevu wa kontena
349.
“Tuliagizwa tuwakamate watumishi watano, mpaka sasa tumewakamata wanne,
mmoja ndio tupo kwenye utaratibu wa kumkamata, lakini kikubwa ni kwamba
tumeanza upelelezi, kama tulivyoagizwa,” alisisitiza DCI Diwani.
Home
/
MATUKIO
/
Moto Wa Magufuli Watua Kwa Bakhresa.......TRA Yazuia Makontena Yake Bandari Kavu, Kampuni Yake Yahusishwa na Ukwepaji Kodi
Moto Wa Magufuli Watua Kwa Bakhresa.......TRA Yazuia Makontena Yake Bandari Kavu, Kampuni Yake Yahusishwa na Ukwepaji Kodi
Tagged with: MATUKIO
Hakuna maoni :