Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema yuko tayari
kukamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka, kama kitendo chake
cha kujitangazia ushindi ni kosa.
Maalim Seif alikuwa akizungumza na viongozi wa majimbo, makatibu wa
matawi, wajumbe wa mkutano mkuu, wajumbe wa kamati za utendaji za ngazi
zote na watendaji wa chama hicho.
Alisema haoni hatua yake ya kuitaka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC)
imtangaze kuwa mshindi haina matatizo kwa kuwa ana uhakika kuwa ndiye
aliyeshinda kwenye uchaguzi.
“Nilichosema ni ZEC initangaze kwa kuwa
nilishinda uchaguzi. Je, hapo kuna ubaya gani ati? Nishitakini basi,
nasema niko tayari, nishtakini. Nitakuja mahakamani kujitetea, mnamtisha
nani! Mnamtisha nani hapa?” alihoji.
Maalim Seif aliwania urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF akiungwa mkono
na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), akichuana
vikali na mgombea wa CCM, Dk Mohamed Shein.
Hadi sasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) haijamtangaza
mshindi na badala yake imefuta matokeo ya kura za nafasi hiyo pamoja na
za uchaguzi wa wawakilishi, ikisema uchaguzi utarudiwa tena ndani ya
siku 30.
Hata hivyo, CUF imepinga ikitaka ZEC imtangaze mshindi kwa madai kuwa chama hicho ndicho kilichoibuka na ushindi.
Jana, Maalim Seif, ambaye ameshagombea urais wa Zanzibar mara tano,
alirudia wito wake wa kuitaka ZEC imtangaze kuwa mshindi ili aapishwe na
kuanza kazi, ikidai anataka kuanza kuijenga upya Zanzibar. Pia
alisisitiza msimamo wake wa kushirikiana na CCM katika utawala wake kwa
kuwa Katiba ya Zanzibar inaelekeza chama kinachoshinda kuunda Serikali
ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
“Sijui wenzetu wanachohofia ni nini na mara
hii sisi (CUF) tumeshinda viti 27 na wao idadi hiyo hiyo ya viti 27 vya
Baraza la Wawakilishi, tutakuwa na idadi sawa kwa sawa ya mawaziri
tuongoze nchi pamoja,” alisema Maalim Seif.
Kiongozi huyo wa CUF alihoji sababu za Rais Shein kutokubali kushindwa akihoji anaona ubaya gani kuridhia.
“Tukae pamoja tuunde Serikali akiwa Makamu wa
Kwanza wa Rais au kama hataki CCM wamteue mtu yoyote tuongoze nchi.
Mbona mimi niliridhia kuwa Makamu wa Kwanza?” alihoji.
Maalim Seif alisema hakuna namna yoyote ya kupindua uamuzi wa wananchi walioufanya kupitia masanduku ya kura.
Alisema wanachokifanya ZEC ni kuchelewesha kukamilisha uhakiki wa kura
kwa majimbo 14 yaliyobakia na kumtangaza mshindi wa urais, na hivyo
kuishauri ZEC kukamilisha kazi ili serikali mpya ianze kufanya kazi ya
watumikia wananchi.
Alisema tayari dunia nzima wanamfahamu rais aliyechaguliwa na wananchi
wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu uliopita, na kuwataka wanachama wa CUF
kuacha kusikiliza kile alichokiita proganda za CCM zinazoeleza kurejewa
kwa uchaguzi.
Akizungumzia madai ya ongezeko la kura katika kisiwa cha Pemba, Maalim
Seif alisema hayo hayana ukweli kwani hakuna hata ‘kituo kimoja
kilichozidishwa wapiga kura 350 kama ZEC ilivyopanga, akisema vingine
vilikuwa na wapigakura chini ya idadi hiyo.
Mapema akizungumza katika mkutano huo, mkurugenzi wa mipango na uchaguzi
wa CUF, Omar Ali Shehe alisema chama hicho kimepata ushindi mkubwa kwa
nafasi za uwakilishi na udiwani.
Alisema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 chama hicho kilipata
wawakilishi wanne na madiwani saba kisiwani Unguja, lakini katika
uchaguzi wa 2015 kimepata wawakilishi tisa na madiwani 15.
Kiongozi huyo alisema CCM imepoteza kata zote tatu za udiwani katika
kisiwa cha Pemba na kukifanya chama hicho kushindwa kupata mjumbe katika
Baraza la Wawakilishi, ubunge na udiwani.
Kabla ya mkutano huo, alielezea kauli ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi
la CUF kilichokutana chini ya mwenyekiti wake, Twaha Taslima, akisema
kiliishauri ZEC kutengua uamuzi wa mwenyekiti wake, Jecha Salim Jecha wa
kufuta uchaguzi mkuu wa Zanzibar, kwa vile hana mamlaka ya kikatiba na
wala Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar hampi nguvu ya kufuta uchaguzi huo.
Jecha amekuwa akidaiwa kufanya uamuzi huo bila ya kushirikisha viongozi wenzake wa ZEC.
Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, matokeo ya uchaguzi wa
Rais yanatakiwa kutolewa siku tatu baada ya wananchi kupiga kura na
yanaweza kucheleweshwa kwa siku tatu zaidi iwapo kutatokea matatizo
katika kuhesabu kura.
Tagged with: SIASA
Hakuna maoni :