Baada ya Rais John Magufuli kuanza kwa kishindo maisha ya Ikulu kwa
kutekeleza kauli mbiu yake ya “hapa kazi tu”, watu walioongea na gazeti
hili wameonyesha kuridhishwa, lakini baadhi wakimpinga na wengine
kumkosoa.
Akiwa kwenye kampeni za kuutaka urais kwa tiketi ya CCM, alisema ataanza
kazi mara baada ya kuapishwa, na atafanya kazi usiku na mchana.
Katika siku nne za kwanza, Rais huyo wa Serikali ya Awamu ya Tano pia
ametoa maagizo kadhaa, ikiwemo kuitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
kuhakikisha inakusanya kodi hasa kwa kuwabana wafanyabiashara wakubwa,
kuziba mianya ya ukwepaji kodi na kutangaza elimu bure kuanzia mwakani.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo baada ya kufanya kikao na makatibu
wakuu, naibu makatibu wakuu, Gavana wa Benki Kuu Prof. Benno Ndulu na
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade kwa lengo
la kutoa mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Alisema mabalozi wa Tanzania wanaowakilisha nchi huko nje, ndiyo
watakaotakiwa kufanya shughuli zote kwenye nchi wanazofanya kazi hadi
hapo atakapolitolea suala hilo uamuzi mwingine.
Wasemavyo wasomi
Wengi waliozungumza na gazeti hili walimsifu Rais Magufuli kutokana na
kuagiza walipa kodi, hasa wafanyabiashara wakubwa wadhibitiwe,
kusimamisha safari za nje, wakisema fedha zitakazookolewa zitasaidia
katika kutekeleza ahadi ambazo yeye na chama chake walizitoa wakati wa
kampeni.
“Ingawa kitaalamu huwezi kupima utendaji kwa siku tatu, Rais Magufuli
ameanza kazi kwa kutoa maagizo ili kuhakikisha anatekeleza aliyoahidi
kama kutoa elimu bure ya msingi hadi sekondari,” alisema Profesa Lugano
Kusiluka wa Chuo Kikuu Huria (OUT).
“Sasa ni wajibu wa watendaji wa serikali kutekeleza.”
Sifa kama hizo zilitolewa na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Charles
Marwa, ambaye alisema hatua ya kuanzia kuwabana walipa kodi wakubwa ni
mwanzo mzuri, akishauri Dk Magufuli aanze kuwabana maafisa wa juu wa TRA
ndipo ashuke kwa maafisa wa chini kudhibiti kodi.
Suala la kodi pia lilizungumziwa na Dk Alexander Makulilo wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam ambaye alisema baadhi ya wafanyabiashara wakubwa ndiyo
wakwepaji wakubwa wa kodi.
“Wakati wafanyakazi wenye mishahara mikubwa ndiyo wanaolipa kodi kubwa
serikalini, baadhi ya wafanyabiashara wakubwa ndiyo wanaoongoza kukwepa
na kusamehewa kodi,” alisema.
Alitaka juhudi kubwa ifanyike katika kuhakikisha wafanyabiashara hao hawakwepi kodi wala kupewa misamaha.
Kwa upande wake, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, George Shumbusho
alisema Dk Magufuli ameanza kazi vizuri kutokana na kuchukua hatua
zinazolenga kuhakikisha Serikali inakuwa na fedha.
Alisema chama chake cha CCM kilitoa ahadi nyingi kwa wananchi wakati wa
kampeni na hivyo ili kutimiza ahadi hizo ni lazima kodi zikusanywe na
kubana matumizi ya Serikali.
Dk Benson Bana, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, pia alipongeza
uamuzi wa kudhibiti walipa kodi akisema kama kila mmoja angekuwa
analipa, nchi isingekuwa na utegemezi katika bajeti kama uliopo sasa.
“Wafanyabiashara wengi hawalipi kodi, wanashirikiana na wafanyakazi
wenye dhamana ya kukusanya kodi kukwepa kodi, wanagawana fedha za
Watanzania. Kama Rais Magufuli ameliona hilo, basi huo ni mwanzo mzuri,”
alisema.
Dk Bana pia alisema Rais anatakiwa kuangalia eneo la matumizi ya magari
kwa watumishi wa Serikali na kushauri walipwe posho ya mafuta badala
kutumia magari ya kifahari ambayo alisema yanatafuna fedha nyingi za
walipa kodi.
“Wanaotakiwa kutumia magari ya Serikali ni mawaziri na manaibu wao,
makatibu wakuu, manaibu wao na wakurugenzi waandaliwe utaratibu mwingine
wa kupewa posho ya usafiri ili watumie magari binafsi,” alisema.
Alisema hivi sasa inawezekana bosi akawa anaishi Bunju na dereva wake
Mbagala ambako ndiko gari linakolala, hali ambayo alisema inasababisha
kuwa na gharama kubwa za uendeshaji.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, George Shumbusho alisema iwapo
Serikali ya Dk Magufuli itawategemea wafanyabiashara wadogo walipe kodi,
haitaweza kutekeleza ahadi zake kwa sababu hakutakuwa na fedha.
Edward Porokwa, ambaye ni mkurugenzi wa shirika la PINGOs Forums,
alisema kutaka walipakodi wakubwa walipe kodi, ni jambo zuri ambalo
litaondoa misamaha ya kodi inayoliangamiza taifa.
Safari za nje hazina tija
Wachambuzi hao pia waliangalia agizo la kusitisha safari za nje hadi kwa
kibali maalumu na kutaka shughuli ambazo zingefanywa na watendaji
waliopo hapa nchini, zifanywe na mabalozi.
“Mabalozi sasa watakuwa na majukumu zaidi katika kuwakilisha nchi nje,” alisema Martine Masawe, mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe ambaye alimsifu Rais kwa uamuzi wa kusitisha safari za nje.
Alisema njia hiyo itapunguza matumizi makubwa ya nchi na kufanya fedha
kuwa na matumizi katika masuala ya kusaidia vipaumbele vilivyopo.
Maoni hayo yanalingana na ya Dk Alexander Makulilo wa Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam (UDSM)aliyesema safari za nje zimekuwa zikitumia fedha nyingi
za walipakodi wakati kuna mabalozi wanaowakilisha nje ya nchi.
“Nashauri yeye ndiye awe mfano kwa kupunguza
safari zake nje kwa sababu Rais na ujumbe wake hutumia gharama kubwa
katika safari za nje,” alisema.
Lakini Dk Bana alikwenda mbali zaidi kwa kusema Rais anatakiwa
kushikilia msimamo wake kwa kuwa suala la safari za nje limekuwapo tangu
Serikali ya Awamu ya Kwanza.
“Ikulu ndiyo ilikuwa inatoa vibali kwa watumishi wanaosafiri kwenda nje
ya nchi, lakini usimamizi umekuwa mbaya na kusababisha watumishi
kusafiri mara kwa mara nje ya nchi kwenye mikutano ambayo wakifika wala
hawachangii chochote,” alisema Dk Bana ambaye amebobea kwenye sayansi ya
siasa.
“Ameanza kazi vizuri kwa sababu eneo la safari
za nje linapoteza fedha nyingi wakati watumishi wengi wanakwenda huko
kwa ajili ya kufanya manunuzi.”
Pia Faraja Christotoms, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm),
alimtahadharisha kuwa maagizo hayo yasiwe nguvu ya soda.
“Kasi aliyoanza nayo siyo mbaya, tunaomba tu isiwe kama nguvu ya soda,” alisema.
“Hata Rais (wa Serikali ya Awamu ya Nne,
Jakaya) Kikwete alianza hivyo hivyo kwa kutembelea wizara mbalimbali.
Lakini hawa ni watu wawili tofauti. Tumpe muda tuone, labda ana dhamira
nzuri na nchi yake.”
Hoja za wanaomkosoa
Maagizo na utendaji wa Rais katika siku zake nne za kwanza hayajakosa wakosoaji.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Paul Losolutie alisema agizo
la kutoa elimu bure linahitaji kwenda sambamba na vifaa vya elimu.
“Hata kama watasema elimu bure wakati bado shule hazina madawati na
walimu hawalipwi vizuri itakuwa haina maana kusema elimu ni bure wakati
wanafunzi katika fomu zao za kujiunga na shule wataambiwa waje na
mchango wa maabara, madawati, mafyekeo, walinzi na majembe,” alisema.
Alishauri utekelezaji wake uwe ni pamoja na kufuta michango ya wazazi,
akisema kwa sasa ada ya shule hizo ni Sh 20,000, lakini michango ya
mwanafunzi anayeingia kidato cha kwanza inafikia Sh300,000 jambo ambalo
ni mzigo kwa mzazi kuliko ada.
Mwanafunzi wa Chuo cha Mipango Dodoma, Godrick Ngoli, alisema uamuzi wa
kutoa elimu bure ni mzuri, lakini ingefaa zaidi baraza la mawaziri
kushirikishwa kwanza ili kupanga mipango ya utekelezaji wake kwa pamoja.
Mwingine aliyemkosoa ni Profesa Semboja ambaye alisema Dk Magufuli
alitakiwa kwanza kuhakikisha mifumo yote ya Serikali inafanya kazi
vizuri kwa namna inavyotakiwa.
Alisema iwapo Rais atafuatilia kila kitu, itafikia wakati atachoka na kuona mzigo mkubwa.
Alimshauri atumie siku 100 za kwanza kusoma mifumo inavyofanya kazi na
kuwapa majukumu watendaji wake ili kurekebisha kasoro atakazokuwa
amezibaini.
“Urais ni taasisi, na siyo kwamba Rais
atafanya kila kitu mwenyewe. Rais Magufuli ahakikishe anakuwa na timu
nzuri ya watendaji ambayo itamsaidia kusimamia yale yote anayotaka
yafanyike bila yeye kusema neno,” alisema.
Pia, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Paul Rosolutie alitilia shaka
utekelezaji wa elimu bure na kusema suala hilo linahitaji muda wa
kutosha ili kuweka mipango ya utekelezaji wake bila kuathiri huduma
nyingine muhimu kwa shule za umma.
“Hata zile Sh20,000 wanazolipa wanafunzi
zilikuwa hazitoshi kutatua matatizo ya shule na Serikali inashindwa
kupeleka fedha za wanafunzi. Sidhani kama hilo lilifanyika, vinginevyo
itakuwa ni mzigo mkubwa kwa watendaji wa Serikali katika kulitekeleza,” alifafanua.
Wapinga kusitishwa safari
Marwa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe pia alipinga uamuzi wa kusitisha safari
za nje akisema utasababisha matatizo kwa kuwa makubaliano mengi ya nchi
huhusisha mawaziri na watumishi wa Serikali.
“Sasa kusema mabalozi ndiyo watakuwa wanawakilisha nchi katika baadhi ya mambo haitawezekana,” alisema.
Marwa alitoa mfano Rais aliyepita aliyesitisha safari zote za nje
isipokuwa kwa kibali cha Serikali wakati akiingia madarakani mwaka 2005,
lakini akakumbana na ugumu katika utekelezaji wa agizo hilo, na badala
yake safari zikaongezeka.
Maoni ya wananchi
Wananchi wengine walioongea na Mwananchi pia walisifu hatua ambazo Dk Magufuli ameshachukua hadi sasa.
Mwenyekiti wa Kampuni za Ulinzi, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kasimir
Kubaja alisema kuzuia safari za viongozi nje ya nchi ni safi kwa sababu
zinatumia fedha nyingi za kigeni wakati ukweli wapo mabalozi ambao
wangeweza kutekeleza majukumu hayo.
Hata hivyo Kubeja alimshauri Rais Magufuli kufuatilia kwa ukaribu suala
la wazabuni serikalini akisema fedha nyingi zinaibwa katika manunuzi.
Naye mhandisi wa umeme wa mjini Mbeya, George Mwang’ombe alisema kitendo
cha kusitisha safari za nje kwa viongozi ni kizuri, lakini kiende
sambamba na kupiga marufuku magari ya Serikali kwenda kwenye baa, kuzuia
posho za vikao vya ndani na kuwabana watendaji wa halmashauri wafanye
kazi za wananchi.
Mwang’ombe pia alishauri Serikali itoe fedha za uendeshaji kwenye shule
za sekondari na za msingi ili kuepusha ukata utakaosababishwa na
kutolewa elimu bure.
Mkurungezi wa asasi ya Kukuza Utawala na Uwazi Tanzania (IGT), Edwin
Soko alisema Rais amefanya vizuri kufuta safari za nje na kwamba njia
hiyo itamfanya aweze kutimiza ahadi zake, kama kutoa Sh50 milioni kwa
kila Kijiji, kujenga barabra za kisasa pamoja na kununua meli mpya.
Ofisa Ustawi wa Jamii, Mwanza, Davis Justine alisema Dk Magufuli
amefanya vizuri kuagiza wafanyabiashara wakubwa wabanwe na kulipaa kodi
na kufuta safari za nje, kwa kuwa zilikuwa zinapoteza fedha nyingi
ambazo zingewekezwa katika sehemu nyingine zingeleta maendeleo.
Sharon Sauwa, Lauden Mwambona, Lilian Lucas, Ngollo John, Peter Elias, Mussa Juma na Raymond Kaminyoge.
Tagged with: SIASA
Hakuna maoni :