Wakati Serikali ikikunjua makucha yake dhidi ya wote waliohusika katika
kashfa ya kupitisha makontena 349 kwenye Bandari ya Dar es Salaam bila
ya kuyalipia kodi, imefahamika kuwa idadi hiyo ya makontena ni sehemu
ndogo tu ya mamia ya mizigo yanayovushwa kinyemela kila uchao na
kuikosesha serikali mabilioni ya fedha.
Hata hivyo, wakati serikali ya Rais Magufuli na Waziri Mkuu wake, Kassim
Majaliwa, ikiendelea kutafuta suluhu ya kudumu kuhusiana na ukwepaji
kodi, imebainika kuwa kazi hiyo siyo lelemama kwani zipo njia zaidi ya
tisa zinazotumiwa kukwepa kodi katika Bandari ya Dar es Salaam.
Mosi, ni kupitia mwanya utokanao na mfumo wa zamani wa malipo usiohusisha ule wa sasa wa kielektroniki, maarufu kama ‘E-Payment’.
Kwamba, wafanyabiashara wengi hutumia mfumo huo wa zamani unaohusisha
matumizi ya karatasi zilizojazwa kwa mkono na hivyo kuwezesha ujanja wa
kubadili taarifa kwa manufaa ya mitandao ya wakwepaji wa kodi.
“Tatizo lililopo ni kwamba mfumo wa E-Payment ni mpya (umeanza Julai) na
umefungwa kwenye benki moja tu iliyopo ndani ya eneo la Bandari… ule wa
zamani unaendelea kutumiwa na wajanja hucheza na maandishi ya kujaza
kwa mkono kuhujumu mapato ya serikali,” chanzo kimeeleza.
Njia ya pili ya kuhujumu mapato bandarini hapo, imetajwa kuwa ni
ya kushirikiana na maafisa wa benki. Hii ina uhusiano mkubwa na njia ya
kwanza inayohusisha matumizi ya mfumo wa malipo wa zamani usiokuwa wa
kielektroniki.
Mfanyabiashara anaweza kuandikiwa kodi sahihi anayotakiwa kulipa, lakini
anashirikiana na wafanyakazi wa benki anayokwenda kuweka fedha kwa
kuhakikisha kuwa baada ya kufanikiwa kuondoa kontena bandarini, maafisa
wa benki husika husitisha malipo hayo kwa kuondoa fedha husika kwa madai
kuwa fedha ziliingizwa kwenye akaunti husika kimakosa.
“Huwa kuna ushirikiano wa karibu kati ya maafisa wa benki na
mfanyabiashara husika. Baada ya kontena kutolewa bandarini, hamisho la
fedha (transaction) huondolewa katika mfumo kwa maelezo kuwa halikuwa
sahihi,” chanzo kimedai, huku kikisisitiza kuwa ushirikiano huo
huhusisha pia watu wa Bandari na TRA ambao mwishowe hugawana malipo
kadri wanavyokubaliana.
Tatu, ni mwanya wa uvushaji wa makontena yenyewe yasiyolipiwa
ushuru kupitia mageti maalum yanayofahamika kwa kazi hiyo, hasa geti
Namba 3 ambalo chanzo kimedai ndilo linaongoza kupitisha mizigo ya
‘dili’.
“Kwa ujumla yapo mageti matano ya kupitisha bidhaa mbalimbali, baadhi yakiwa ni ya kupitihia mafuta, nafaka na magari.
"Hili Namba 3 ndiyo hutumika kupitisha makontena ya bidhaa zenye thamani
kubwa na wengi wasiolipa kodi hulitumia hili,” chanzo kilieleza kabla
ya kufafanua kuwa awali, hilo geti Namba 3 halikuwa na mfumo wowote wa
kuangalia kama kontena husika limelipiwa au la na ndiyo maana lilikuwa
likitumika zaidi kupitisha makontena yasiyolipiwa kodi.
Njia ya nne ya kuhujumu kodi ya mapato ni ya kuwatumia watu
wanaoendesha bandari kavu (ICD’s). Inaelezwa kuwa hivi sasa kuna bandari
kavu 12, ambazo kila meli inapoingia hujulikana kila mzigo husika
unapelekwa kwenye bandari ipi kati ya hizo.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa kinachofanyika ni kwa baadhi ya makontena
yanayotolewa bandarini ili yapelekwe bandari kavu kabla ya kukombolewa
na wahusika huishia kupelekwa kwa wafanyabiashara wenye makontena na
hivyo kuikosesha mapato serikali.
“Awali kwenye ICD’s kulikuwa na askari wa mmiliki wa ICD’s na siyo wa
TPA… huyu alikuwa akiangalia malipo ya bosi wake tu ambayo ni gharama za
kuhifadhi mzigo na hivyo TPA na TRA huambulia patupu,” chanzi
kimeeleza, kikiongeza kuwa hivi sasa walau kuna nafuu kwani kwenye ICD’s
kuna walinzi wa TPA lakini hilo limefanyika baada ya watu kuwa tayari
wameshaiba sana.
Njia ya tano inayotumiwa kukwepa kodi ni ya kubadili taarifa,
hasa kupitia watu wenye wajibu wa kufanya tathmini. Kwamba, badala ya
mzigo kukadirwaa kodi kwa kiwango sahihi, wahusika ambao zaidi huwa ni
watu wa TRA hukadiria fedha kidogo baada ya kujihakikishia kuwa nao
wanapewa mgawo na wafanyabiashara.
“Hapo utakuta kontena la kodi ya milioni 80, mteja anaambiwa alipe
milioni 40 tu … na wakati mwingine kiasi hicho pia hakiandikwi balki
huandikwa cha chini zaidi kama milioni 5 tu…hii ni njia nyingine
inayoligharimu taifa mabilioni ya fedha,” chanzo kimeeleza.
Njia ya sita inayofanikisha ukwepaji kodi ni mtandao mpana wa
baadhi ya vigogo wa maeneo mbalimbali Bandarini na TRA, ambao hawa
huhakikisha kuwa wanakuwa na timu ya vijana wao wa kazi karibu katika
kila eneo ili kufanikisha mipango yao.
“Hii ndiyo njia kubwa ya hujuma. Kama utakumbuka aliyekuwa Waziri wa
Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alisambaratisha baadhi ya mitandao kwa
kuwagusa vigogo 27… ile ilikuwa kuvunja mtandao uliokuwapo. Hilo
lilisaidia kiasi, lakini sasa ipo pia mitandao mingine ambayo uchunguzi
ukifanyika utabaini kuwa mambo yameanza kurudi kama zamani,” imeelezwa.
Njia ya saba ya ukwepaji kodi ni kwa baadhi ya vigogo wa Bandari
na TRA kuanzisha kampuni zao za uondoaji mizigo bandarini. Inaelezwa
kuwa hizi hutumiwa sana kufanikisha ‘dili’ za ukwepaji kodi na ndiyo
maana haishangazi kusikia kuwa kuna makontena zaidi ya 300 hayaonekani
kwenye kumbukumbu za TRA.
Njia ya nane ya ukwepaji kodi ni kuonyesha kuwa kontena
linapelekwa nje ya nchi, kwa mfano Malawi, wakati ukweli ni kwamba
huishia hapahapa nchini.
“Utakuta kontena linadaiwa kupelekwa Malawi, lakini linachukuliwa na
gari kukuu linaloonekana wazi kuwa haliwezi kufika hata Kibaha… njia hii
pia hutumiwa sana kuikosesha serikali mapato,” chanzo kingine kilisema
Njia ya tisa ya ukwepaji kodi ni ucheleweshaji wa makusudi wa
utoaji makontena. Kwamba, mteja anapotaka kutoa mzigo wake kwa kufuata
njia halali zilizopo, huishia kuzungushwa kila uchao ili akubali kutoa
rushwa na mwishowe kulipishwa kiwango pungufu cha kodi au kulipa fedha
zisizoingia kabisa kwenye mikono ya TRA.
Njia ya kumi ni ubabaishaji unaofanyika katika kuorodhesha idadi
ya makontena inayotolewa bandarini kwenda kwenye bandari kavu. Hapa,
kama makontena yanayotolewa ni 12, basi huandikwa kuwa ni 10 na mengine
mawili huishia kuondolewa bila ya kuwa na kumbukumbu zake kwa ajili ya
kulipiwa kodi.
Pamoja na kuwapo kwa njia zote hizo, chanzo kimedai kuwa sababu kubwa ya
kufanikiwa kwa ukwepaji kodi ni mtandao mpana unaoundwa na vigogo
mbalimbali na ndiyo maana taarifa mbalimbali za wakaguzi wa ndani na wa
nje katika Bandari ya Dar es Salaam huishia kubaki kwenye makabrasha
bila ya kuwapo kwa utekelezaji wowote wa vitendo juu ya yale
yanayopendekezwa na wataalamu.
Chanzo: Nipashe
Tagged with: MATUKIO
Hakuna maoni :