Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ,
leo mchana amefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili na kukutana na hali ya kumsikitisha.
“ Rais amesikitishwa na kuhuzunishwa na hali ya huduma kwa wagonjwa
hususan wanaolala chini. Pia amekasirishwa na hali ya kutokujali wala
kushughulikia vifaa vya kufanyia kazi ambapo amekuta mashine muhimu za
uchunguzi wa magonjwa kama vile MRI na CT-SCAN zikiwa hazifanyi kazi kwa
muda wa miezi miwili sasa, ilihali mashine kama hizo katika Hospitali
za binafsi zinafanya kazi na wagonjwa wanaelekezwa kwenda kutafuta
huduma huko”. Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema na kutoa
maelekezo yafuatayo :
Rais amevunja Bodi ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambayo
ilishamaliza muda wake na amemteua Prof. Lawrence Mseru , kukaimu nafasi
ya Mkurugenzi Mkuu wa Muhimbili kuanzia kesho tarehe 10 Novemba, 2015.
Dkt. Hussein L. Kidanto ambaye ndiye anayekaimu hivi sasa, amehamishiwa
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambako atapangiwa kazi nyingine.
Balozi Sefue pia amesema, Rais ametoa wiki moja na kwa vyovyote si
zaidi ya wiki mbili kwa uongozi mpya wa Muhimbili kuhakikisha kuwa
mashine zote za uchunguzi wa magonjwa ambazo hazifanyi kazi zinafanya
kazi na kuhudumia wananchi kama ipasavyo.
Tayari Wizara ya Fedha imetoa shilingi bilioni 3 kwa ajili ya kazi hiyo
na kulipa madeni ya ukarabati wa mashine za uchunguzi wa magonjwa
nchini.
Hata hivyo Katibu Mkuu Kiongozi amesema kuanzia sasa hospitali zote
nchini zinatakiwa kutenga fedha kutoka kwenye mapato yao wenyewe na
kuhakikisha mashine na vifaa vyote vya kazi vinafanya kazi wakati wote
(Regular Maintenance).
Balozi Sefue pia metumia nafasi hii kuwaagiza watendaji na viongozi wote
katika sehemu za kazi kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo na
kazi za umma zinatekelezwa ipasavyo.
“Hakutakuwa na huruma kwa watumishi wa Umma wasiojali wananchi na mahitaji yao” Amesisitiza Balozi Sefue.
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu – Dar es Salaam.
9 Novemba, 2015
Home
/
MATUKIO
/
Rais Magufuli Afanya Ziara Ya Kushtukiza Muhimbili..Akuta Hali ya Kusikitisha....Avunja Bodi Ya Uongozi Wa Hospitali, Ateua Uongozi wa Muda
Rais Magufuli Afanya Ziara Ya Kushtukiza Muhimbili..Akuta Hali ya Kusikitisha....Avunja Bodi Ya Uongozi Wa Hospitali, Ateua Uongozi wa Muda
Tagged with: MATUKIO
Hakuna maoni :