Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema nguvu ya
aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa ilivuruga
mpango wake wa kupokea wabunge 50 kabla ya Uchaguzi Mkuu.
Alisema Lowassa aliyekuwa akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) alikuwa na nguvu kubwa kiasi cha kufanya ACT
pia ishindwe kupata wabunge wengi katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika
nchini Oktoba 25.
Zitto alitoa kauli hiyo alipotakiwa kueleza sababu za ACT kushindwa
kutimiza azma yake ya kupokea wabunge 50 kutoka vyama mbalimbali, kabla
ya Uchaguzi Mkuu na kupata wabunge wengi baada ya uchaguzi huo kama
alivyoahidi miezi michache kabla ya kuanza kwa kampeni.
Alibainisha kuwa chama chake kilifanya mazungumzo na wabunge wengi
waliokuwa CCM na Chadema ambao walikubali kujiunga nacho na kushiriki
uchaguzi kupitia chama hicho. Lakini mpango huo ulibadilika baada ya
Lowassa kujiunga na Chadema na baadaye kuwania urais akiungwa mkono na
Ukawa.
“Wabunge wengi walikubali kuungana nasi, wamo wa CCM na wabunge wa
upinzani… lakini upepo wa Lowassa uliwabadilisha na hili tusingeweza
kulidhibiti kwa kipindi kile,” alisema Zitto na kuongeza kuwa:
“Katika mazingira ya kawaida Lowassa ndani ya Chadema ni watu wachache
sana wangekwepa upepo wake. Kwanza haikutegemewa kuwa (Lowassa)
anakwenda wapi. Wapo walioamini kuwa anakuja kwetu (ACT), lakini ukweli
ni kuwa hatukuwa na mazungumzo kati yetu (ACT) na Lowassa, ingawa
kulikuwa na wish (matakwa) ya kuwa na coalition (umoja) kubwa zaidi ya
kuunda kambi ya upinzani.”
Kwa nini ACT haikujiunga Ukawa
Zitto alisema sehemu kubwa ya waliounda ACT walitoka Chadema, hivyo kulikuwa na mazingira magumu ya kufanya kazi pamoja tena.
“Sisi tuliweka sharti moja, katika mazingira yoyote ya kufanya kazi
pamoja, kwa matokeo yoyote yatakavyokuwa, moja ya ajenda ilikuwa
kurejesha miiko ya uongozi jambo ambalo wenzetu hawakuwa tayari
kutangaza mali,” alisema Zitto.
Lakini, mwisho baada ya majadiliano, ACT waliona kwa chama hicho ambacho
kinaanza, kikiingia kwenye muungano na vyama vikubwa kingeweza kumezwa
hivyo ni vizuri kwenda wenyewe ili wapate fursa ya kujitangaza kwa
kuweka wagombea katika kila jimbo.
Ulikuwa uchaguzi wa ovyo
Akitoa maoni yake kuhusu uchaguzi uliopita, Zitto alisema ulikuwa mgumu,
usioeleweka na uliokosa ajenda za wananchi. Badala yake, ulilenga
mapambano ya wagombea na si sera.
“Uchaguzi ulikuwa kati ya CCM na Ukawa, ulikuwa ni kati ya (John)
Magufuli na (Edward) Lowassa. Ulikuwa kuhusu personalities (watu) na
siyo issues (hoja), naweza kusema ulikuwa miongoni mwa uchaguzi wa ovyo
kweli kuwahi kutokea nchini,” alisema Zitto.
Aliongeza kuwa uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa tofauti na wa miaka ya
nyuma kutokana na kuwa wagombea wote wenye nguvu walikuwa ndani ya
mfumo.
“Usingeweza kuwatofautisha wagombea wote waliokuwa au waliotokana na
mfumo uliopo… ilikuwa vigumu kuacha kumfananisha mgombea wa CCM na yule
wa Ukawa, wote ni walewale usingetegemea chochote. Kwa hiyo sisi (ACT)
hata tungejitahidi tusingeweza kufanya kitu ni mara chache sana tulikuwa
tukisikika,” alisema.
Kwa mujibu wa Zitto, uchaguzi uliopita ulikuwa mgumu na usio na ajenda ikilinganishwa na wa mwaka 2010.
“Kumbukeni uchaguzi wa mwaka 2010, vyama vilibishana kuhusu ajenda,
baada ya uchaguzi watu walikuwa na ajenga ya uchaguzi, lakini angalia
sasa wapinzani au vyama wanajadili nini, hakuna,” alisema.
Alisema ajenda ya kupinga ufisadi na rushwa iliyokuwa ikitumiwa na wapinzani, sasa imechukuliwa na Rais Magufuli.
“Sasa watu wanasubiri kusikia Rais atasema nini, watu wamesahau kwamba
hakuna Baraza la Mawaziri, lakini nchi inakwenda… hata ile hoja ya Ukawa
ya kutomtambua Magufuli haipo tena,” alisema.
Upinzani umepoteza
Zitto anasema anachokiona ni wapinzani umepotea kutokana na ajenda yao ya ufisadi kuchukuliwa na Rais Magufuli.
“Sasa unasikia Magufuli anakuwa mkali sana kuhusu rushwa na ufisadi
jambo ambalo zamani halikuwapo naweza kusema tumebadilishana. Zamani
ilikuwa wapinzani wanazungumzia rushwa na CCM wanaitetea Serikali,
lakini sasa majukumu yamebadilika,” alisema.
Alisema kwa sasa sauti ya wapinzani katika hoja haisikiki na badala yake
anasikika Rais Magufuli pekee ambaye amekuwa Serikali na upinzani
wakati mmoja.
“ Hii itaimarisha zaidi demokraia kwa sababu kwa muda mrefu upinzani
umekuwa ukitegemea matukio kujenga au kufanya siasa, itabidi sasa
upinzani uendane na hoja katika siasa… lakini mwisho wa siku tunaangalia
mwananchi anafaidika na nini? ” alihoji.
Nafasi ya wapinzani siasa za Tanzania
Zitto alisema kwa ujumla wapinzani wameanza vizuri kwani licha ya kuwa
anachofanya Rais Magufuli kuhusu rushwa kinaonekana kukonga nyoyo za
Watanzania, ukweli unabaki kuwa CCM imechokwa.
“Upinzani una wabunge wengi sana ndani ya Bunge, 122, kwahiyo tunaweza
kujipanga na kufanya kazi ya kuionyesha Serikali matatizo yake wakati
wote na hiki ndicho tulichokuwa tukifanya…Lakini tunayoiona sasa hivi ni
kuwa hatujui, je, nguvu ya Magufuli, ni yake peke yake au ni nguvu ya
taasisi? Na kama ni yake CCM itakuwa ni ile ile na mashambulizi dhidi ya
CCM yatakuwa yaleyale,” alisema.
Mtazamo wake kwa Rais Magufuli
Zitto anamwona Rais Magufuli kama kiongozi aliyekosa msingi, kwani
alichaguliwa bila makundi, hivyo kila anachofanya kinapaswa
kuwafurahisha wananchi ili apate kuungwa mkono.
Alisema kwa muda mrefu wabunge walionekana kuwa na nguvu kwa kuwa pale
Bunge lilipokuwa likipambana na Serikali, wananchi walikuwa nyuma ya
Bunge, lakini sasa hali inaweza kuwa tofauti.
“Kwa namna ya uongozi wa Magufuli, Bunge linaweza kukosa nguvu kwani
likijaribu kumkwamisha atatetewa na wananchi. Wakimpinga (Magufuli)
wananchi watawapinga (wabunge). Na Magufuli alivyo anaweza kusema
turudini kwenye uchaguzi, maana akivunja Bunge tunarudi kwenye uchaguzi
kwani ana uhakika yeye atashinda, lakini wabunge hawatakubali kuingia
kwenye gharama za uchaguzi tena.”
Tutampima Magufuli kwa posho
Wabunge wanataka kukopeshwa Sh 130milioni badala ya Sh90milioni, je Zitto anasemaje?
“Tumuangalie, Je, atasalimu amri kwa shinikizo la wabunge la kuongezewa
mkopo wa gari au atatia mguu kwenye kiasi ambacho wabunge walilipwa
mwaka 2010… akisalimu amri ina maana ni mtu ambaye atataka ushirikiano
na Bunge, lakini akitia mguu ina maana ana msimamo,” alisema na
kuongeza: “Wabunge huwa wanakimbilia kusema tutazuia bajeti, Je,
atatishika. Bado tuna muda wa kutosha wa kuweza kumsoma Magufuli na
kuona ni jinsi gani wanakwenda.”
Kuna uamuzi ambao tayari ameanza kuhusu kurejesha mashamba ambayo
hayajaendelezwa, lakini lipo suala la viwanda. Je, anafanya nini kuhusu
nguo kutoka nje, kuna ukwepaji mkubwa sana wa kodi na viwanda vya
Tanzania,
Zitto anaenda mbali kwa kusema kwa Rais wa aina ya Magufuli ni lazima
kuwe na namna ya kumdhibiti kwani Watanzania watajikuta wanatengeneza
‘dikteta’.
Alisema ili kuendana na kasi ya kiongozi huyo wa nchi, inatakiwa kuwa na Bunge imara.
“Bunge ni lazima libadilike, liache kushambulia watu na badala yake
lijikite kwenye hoja na kwa jinsi Magufuli alivyo wapo wabunge wengi
wataathirika na maamuzi yake… wapo wabunge ambao wapo kwenye matukio ya
rushwa, wafanyabiashara ambao wataguswa na maamuzi yake, kwa hiyo kwa
mwaka mmoja tutashuhudia mengi, ” alisema.
Home
/
SIASA
/
Zitto Afunguka..Asema Nguvu ya Lowassa ilikuwa Kubwa Sana Kiasi cha Kuwavurugia ACT Wazalendo Katika Uchaguzi
Zitto Afunguka..Asema Nguvu ya Lowassa ilikuwa Kubwa Sana Kiasi cha Kuwavurugia ACT Wazalendo Katika Uchaguzi
Tagged with: SIASA
Hakuna maoni :