Wakati Rais John Magufuli akianza kuchukua hatua za kudhibiti matumizi
ya Serikali, wasomi na wanasiasa wamemtajia mambo 14 ambayo wamesema
akiyazingatia atalinusuru Taifa dhidi ya gharama zisizo za lazima.
Mara baada ya kuapishwa, Rais huyo wa Serikali ya Awamu ya Tano alianza
kazi kwa kutembelea Wizara ya Fedha, baadaye kuagiza Mamlaka ya Mapato
(TRA) kudhibiti wakwepa kodi kabla ya kusimamisha safari zote za nje
hadi kwa kibali maalumu.
Dk Magufuli amechukua hatua hizo, ikiwa ni mkakati wa kukusanya mapato
na kudhibiti matumizi kwa lengo la kuijengea Serikali uwezo wa
kuwatumikia wananchi, ikiwa ni pamoja na kutekeleza ahadi ya kutoa elimu
bure hadi kidato cha nne ambayo inahitaji uwezo mkubwa wa kifedha.
Lakini wasomi na wanasiasa wanaona kiongozi huyo wa nchi anatakiwa
kuchukua hatua zaidi kwa kuangalia maeneo mengine ambayo yatasaidia
kuiwezesha Serikali kupata fedha nyingi iwapo atayazingatia.
Akiandika kwenye ukurasa wake wa facebook, kiongozi wa chama cha ACT
Wazalendo, Zitto Kabwe (pichani) alitaja mambo kumi muhimu ambayo
yataisaidia Serikali ya Magufuli kuweka misingi ya mabadiliko ya kweli
katika kipindi cha uongozi wa serikali.
Zitto alimtaka Rais Magufuli kuweka wazi mikataba yote ya rasilimali za
nchi, kufuta posho za vikao katika mfumo mzima wa Serikali kama Mpango
wa Maendeleo unavyotaka na kufuta malipo ya daraja la kwanza kwa usafiri
wa anga kwa watendaji wa Serikali na wanasiasa isipokuwa Rais, Makamu
wa Rais na Waziri Mkuu.
Mwenyekiti huyo wa zamani wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)
pia alitaka kufuta matumizi ya magari ya kifahari, kufuta uagizaji wa
sukari kutoka nje na kuanzisha miradi ya miwa, kuweka wazi taarifa ya
Serikali kuhusu utoroshaji wa fedha na kufungua mashtaka kwa wahusika,
kuipa Takukuru mamlaka ya kukamata na kushtaki, na kila mwenye mali
athibitishe kaipataje.
”Jambo la nane ni kuweka wazi mali na madeni
ya viongozi kwa umma kisha wananchi waruhusiwe kuhoji, kuruhusu mshindi
wa uchaguzi Zanzibar atangazwe na akubali kufanya naye kazi na kuendelea
na mchakato wa Katiba kwa kuanzia alipoishia Warioba, achana na Katiba
Pendekezwa,” alisema mbunge huyo wa Kigoma Mjini.
Kama vile haitoshi, Profesa Humphrey Mushi wa Idara ya Uchumi ya Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alitaja mambo mengine kuwa ni kuepuka
kununua maziwa kutoka nje na badala yake nguvu iwekezwe kwenye viwanda
vya maziwa vya ndani, hasa vilivyopo Tanga na Arusha. Alisema hatua hiyo
itasaidia kuongeza mapato ya ndani na soko la ajira nchini.
“Lakini pili, serikali inatakiwa kuachana na
manunuzi ya samani za ndani kutoka China na Malyasia. Kwanza hazina
ubora na gharama zake ni kubwa kwa hivyo lazima kuwekeza katika manunuzi
ya samani za ndani. Hii itasaidia kupunguza matumizi ya serikali,” alisema Profesa Mushi.
Jambo jingine ambalo msomi huyo alitaja ni udhaifu katika Sheria ya
Manunuzi ya Umma, ambayo alisema inatoa mwanya kwa watumishi wa Serikali
kula rushwa. Alisema udhaifu huo hufanyika wakati wa Serikali
inapotakiwa kulipia kiwango cha riba ya bidhaa katika manunuzi yake.
“Lakini hata kitengo cha manunuzi kimekosa
watalaamu wazuri. Wananunua vifaa visivyokuwa na ubora kwa hivyo ni
hasara kwa Serikali. Ni muhimu kuangalia hilo,” alisema Profesa Mushi.
Alitaja jambo la nne kuwa ni matumizi ya mitambo ya umeme kupitia
kampuni binafsi kwani serikali inaweza kununua mitambo yake na kuepuka
gharama. “Kwa mfano, Serikali inalipa mabilioni ya fedha katika
uzalishaji umeme unaofanywa na kampuni za hapa nchini, lakini fedha hizo
ingeweza kununulia mitambo yake kama ingetunza kwa miaka miwili,”
alisema.
Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Lihundi alitaja
mambo mengine kuwa ni matumizi ya muda katika rasiliamali watu. Alisema
kila mtumishi anatakiwa kufanyiwa tathmini ya matumizi ya muda wake wa
kuzalisha katika nafasi aliyopo serikalini.
“Muda ni muhimu sana. Je, anahudhuria kazini
na kutoa huduma ipasavyo. Je, muda wake anaoutumia kazini unaendana na
kasi ya uwajibikaji. Anazalisha kwa kiwango gani? Na matokeo ya
uwajibikaji yatazamwe,” alisema Lihundi.
Lihundi alisema udhaifu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma pia uangaliwe,
pamoja na matumizi ya magari ya kifahari kwa watendaji wa serikali na
kuhakiki hata safari za ndani ya nchi. “Kufuta safari za nje ni sawa,
lakini ajaribu kutazama safari za ndani. Kuna ubadhirifu unafanyika
sana,” alisema.
“Kwa mfano watumishi wizara yote wanakwenda bungeni, lakini kila mmoja anakwenda na gari lake. Kwa nini wasitumie gari moja?” alihoji Lihundi.
Tagged with: SIASA
Hakuna maoni :