Aliyekua
mgombea Urais anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, ameendelea kudai ndiye mshindi kwenye
Uchaguzi Mkuu uliopita na dunia inajua.
Katika
taarifa aliyoitoa jana kwa vyombo vya habari kupitia msemaji wake,
Aboubakary Liongo, Lowassa alisema ushindi wake uliporwa na kupewa mtu
mwingine lakini amewataka Watanzania wasikate tamaa.
Lowassa
pia aliwashukuru Watanzania kwa kumpa kura nyingi wakati wa uchaguzi
huo, kura ambazo alidai kuwa zilimfanya kuongoza dhidi ya wagombea
wengine.
Hata
hivyo, katika uchaguzi huo wa Oktoba 25, Rais John Magufuli ndiye
aliyeshinda kwa kupata kura 8,882,935 (sawa na asilimia 58.46) na
Lowassa kura 6,072,848 (sawa na asilimia 39.97) ya kura zote.
Mwenyekiti
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva alimtangaza Dk.
Magufuli kuwa Rais mteule siku nne baadaye na aliapishwa Novemba 5,
mwaka huu.
Liongo
alisema Lowassa alitoa shukrani hizo juzi jioni katika mikutano ya
hadhara wa kumnadi mgombea ubunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kwenye
kata za Mkonoo na Nodisaito.
“Nawashukuru
sana Watanzania kwa kanipa kura nyingi kabisa. Tulishinda, dunia nzima
inajua na wao wanajua, Watanzania mmeonyesha imani kubwa kwangu,” amekaririwa Lowassa.
“Nawashukuru
sana Watanzania kwa uvumilivu wenu baada ya kushuhudia ushindi wenu
ukiporwa… mlitaka wakati ule nitoe tamko muingie barabarani kudai
ushindi wenu.
“Lakini nawapenda, Watanzania siko tayari kuona mnapoteza maisha,” imesema taarifa hiyo ikimkariri Lowassa.
Aliwaomba
wananchi wa Arusha kumchagua Lema katika Uchaguzi wa jimbo hilo kesho
ili kuliletea maendeleo Jiji la Arusha ambalo linaongozwa na Ukawa.
Hakuna maoni :