Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amezungumzia kasi aliyoanza nayo
rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli pamoja na
baraza lake la mawaziri.
Akizungumza jana na mwandishi wa habari wa Azam TV, Mbowe alisema kuwa
rais Magufuli ameanza vizuri kiutendaji na kwamba ameanza kuzifanyia
kazi hoja zilizokuwa zikihubiriwa na Chadema ndani na nje ya Bunge.
“Hoja ya kubana matumizi ya serikali, hoja ya kupunguza sherehe za
kitaifa, hoja ya kupunguza safari za nchi za nje kwa viongozi wetu, hoja
ya kupunguza watumishi wa umma ambao hawana umuhimu, hoja ya kuwa na
serikali ndogo. Haya mambo tulizungumza siku zote na hawa hawa wa Chama
cha Mapinduzi ndio waliokuwa wanayapinga haya,” alisema Mbowe.
Mbowe alieleza kuwa dhana ya upinzani sio kupinga kila kitu
kinachofanywa na serikali hivyo chama chake hakitakuwa tayari kupinga
mambo mema yanayofanywa na serikali ya awamu ya tano kama baadhi ya watu
wanavyotarajia, bali kitajikita katika kujadili na kuibua hoja za
msingi.
“Kuwa mpinzani sio kupinga kila jambo linalofanyika hata kama likiwa
jema. Sasa sisi kama kambi rasmi ya upinzani bungeni na hata nje ya
bunge ni wajibu wetu katika wakati wote ule kuhakikisha tunaisimamia
serikali ili anachokisema rais kweli kitekelezwe kwa vitendo na isiwe
hoja ya rais pekee,”alisema.
Hata hivyo, Mbowe alikosoa uteuzi wa baadhi ya mawaziri katika baraza la
serikali ya awamu ya tano hususan Dk. Harison Mwakyembe ambaye wizara
ya Uchukuzi aliyokua akiiongoza awali imekumbwa na sakata la upotevu wa
makontena bandarini na Profesa Sospeter Muhongo ambaye amerudishwa
katika wizara ya Nishati na Madini baada ya kujiuzulu katika nafasi hiyo
wakati wa serikali ya awamu ya nne kufuatia sakata la Escrow.
Hakuna maoni :