Huku
mmiliki wa Klabu ya TP Mazembe, Moise Katumbi, akiendelea kumbania
mshambuliaji wa Tanzania, Mbwana Samatta kujiunga na Genk ya Ubelgiji,
straika huyo amepanga kuununua mkataba wake uliobakia katika timu hiyo.
Taarifa
hizo zimekuja huku kukiwa na madai kuwa Genk iliamua kwenda kushtaki
kwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kuhusu thamani ya muda wa
mkataba wake uliobaki ambapo unatarajiwa kumalizika Aprili, mwaka huu.
Samatta
ameshasaini mkataba wa awali na timu hiyo ya Ubelgiji na mpango wake
kwa sasa ni kuona anaondoka katika timu hiyo yenye makazi yake katika
Jiji la Lubumbashi, DR Congo.
Chanzo
cha uhakika kutoka kwa mtu wa karibu na Samatta, kilisema kuwa mpango
wa straika huyo kwa sasa ni kununua mkataba wake uliobaki ndani ya timu
hiyo ambapo suala hilo tayari ameshamfikishia wakala wake ambaye yupo na
mwanasheria kwa ajili ya kulifanyia mchakato jambo hilo.
“Genk
wamekwenda Fifa kushtaki lakini kwa upande wa Samatta, amemuagiza wakala
wake akae na mwanasheria kwa lengo la kujadili jinsi ya kununua mkataba
wake uliobaki ili aweze kuondoka,” kilisema chanzo hicho.
Kwa
upande wa meneja wa mchezaji huyo, Jamali Kisongo alipoulizwa kwanza
alikiri kuwepo kwa mpango huo wa kununua mkataba uliobaki kwa kuwa
hawafikirii kukubali mchezaji kurejea Mazembe.
“Ni
kweli huo mpango wa kununua sehemu ya mkataba wake upo, umeshaanza
kufanyiwa kazi kupitia wakala na mwanasheria wake licha ya Genk kwenda
Fifa, lakini sisi tunaangalia namna ya kuweza kulishughulikia kwa sababu
hata atakaporejea kutoka kwenye tuzo huko Nigeria, tutasafiri kwenda
Ubelgiji kukamilisha mambo yaliyobakia likiwemo suala hilo la mkataba,”
alisema Kisongo.
Hakuna maoni :