Uchaguzi wa marudio wa Zanzibar ambao umepangwa kufanyika
Machi 20, mwaka huu, umesababisha Chama cha wananchi (CUF) kushindwa
kufanya maadhimisho ya kuwakumbuka wenzao waliofariki dunia mwaka 2001.
Maadhimisho hayo hufanyika Januari 27 ya kila mwaka yakishirikisha viongozi wakuu wa chama hicho pamoja na wafuasi wake.
Akizungumza na Nipashe jana, Naibu Mkurugenzi wa Habari na
Uenezi wa chama hicho Taifa, Abdul Kambaya, alisema uongozi wa CUF taifa
hautafanya maadhimisho hayo kwa kuwa siku hiyo Kamati Ttendaji itakuwa
inafanya kikao cha kujadili tarehe ya marudio ya uchaguzi ambayo
ilitangazwa hivi karibuni na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec).
Kambaya alisema siku hiyo kamati itakutana kuandaa ajenda
kuhusiana na kutangazwa kwa tarehe hiyo ya uchaguzi ambazo zitapelekwa
katika Baraza Kuu la chama.
“Ni vijana tu ndiyo watafanya maadhimisho hayo kwa upande
wa Zanzibar na ndiyo ambao watafanya maandamano ya kukumbuka mauaji
hayo.”
Maandamano hayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka kama
kumbukumbu ya kuomboleza vifo vya wafuasi wa chama hicho waliouawa
Januari 27, mwaka 2001 wakati wa maandamano ya kupinga matokeo ya urais
visiwani humo.
Hakuna maoni :