Mwanasheria Mkuu (AG) wa zamani
Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema Rais wa Zanzibar, Dk. Ali
Mohammed Shein, anapaswa kujiuzulu kwa sasa na Jaji Mkuu kuiongoza
visiwa hivyo kwa kuunda kamati maalum itakayochunguza uhalali wa kufutwa
kwa matokeo ya uchaguzi mkuu visiwani humo.
Aidha, amesema Rais Dk. John Magufuli anapaswa
kuingilia kati mgogoro uliopo visiwani humo, ili kuinusuru nchi kuingia
katika mgongano wa kisiasa.
Aliyasema hayo jana wakati wa
kongamano la wazi juu ya changamoto za kisheria zilizojitokeza baada ya
kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana,
lililoandaliwa na Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS), jijini Dar es
Salaam jana.
Alisema Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu,
anapaswa kuingoza Zanzibar kwa sasa na kuunda tume huru itakayochunguza
uhalali wa kisheria uliosababisha kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo na
kusababisha mvutano wa kisiasa visiwani humo.
Alisema endapo kamati hiyo itabaini kuwa hakukuwa na
uhalali wa kufutwa kwa uchaguzi huo, waliohusika kufutwa watatakiwa
kufikishwa katika mikono ya sheria.
Source: Nipashe
Hakuna maoni :