SIKU chache baada ya Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Boniface Mkwasa
kumtangaza mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika, Mbwana Samatta,
kuwa nahodha mpya wa timu hiyo, aliyekuwa nahodha, Nadir Haroub
‘Cannavaro’ alitangaza kustaafu kuichezea Stars.
Kitendo hicho kimetafsiriwa sivyo ndivyo na wadau wakimuona Cannavaro kama mtu wa kuzira na aliyekurupuka kwa hasira ya kuvuliwa cheo, lakini ukweli ni kwamba mkewe aitwaye Meiya Nadir au Meiya Almasi anahusika na maamuzi hayo ya nahodha huyo wa Yanga.
Akizungumza na Mwanaspoti, Meiya alisema alitoa baraka zote za kustaafu kwa mume wake huyo ndani ya kikosi cha Taifa Stars, kwani alikuwa akimshauri afanye hivyo siku nyingi zilizopita, lakini yeye ndiye alikuwa anagoma.
Meiya amesema lengo hasa la Cannavaro lilikuwa ni kustaafu kikosini hapo baada ya mechi tatu zijazo kutoka ile waliyofungwa mabao 7-0 Algeria, lakini alichukua uamuzi wa kutangaza nia yake hiyo kabla kutokana na shinikizo kutoka kwa jamaa zake wa karibu akiwemo mke wake huyo.
“Cannavaro alitaka kustaafu baada ya mechi tatu na kuwaaga mashabiki wake kwa heshima kama ilivyowahi kufanywa na manahodha wengine waliomtangulia Salum Sued ‘Kussy’, Shadrack Nsajigwa na Mecky Maxime ili kuwaachia damu changa majukumu,” alisema.
“Kustaafu kwake kwangu ni furaha kabisa na mimi ni miongoni mwa waliomshawishi kufanya hivyo kwa sababu lengo langu lilikuwa afanye hivyo siku nyingi tu zilizopita.
“Mimi naona amefanya vizuri tu, muda wa miaka 10 aliochezea Taifa Stars unatosha, awaachie vijana na yeye aendelee na majukumu mengine kama klabu na mambo mengine.”
Cannavaro ni beki wa Yanga, yuko kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa miaka 10 na hakuwahi kuachwa kwa kipindi chote kabla ya wiki iliyopita, kutangaza kustaafu rasmi kikosi hicho na kuacha maswali mengi kwa wadau w mchezo huo unaoshika nafasi ya kwanza nchini.
Hakuna maoni :