Watu watatu wa familia moja, wakazi wa Kijiji cha Mchukwi wilayani hapa
Mkoa wa Pwani, wamekufa baada ya kupigwa na radi jikoni wakati mvua
zikinyesha.
Tukio hilo limetokea jana jioni katika kijiji hicho. Inadaiwa kuwa radi
hiyo ilianza kupiga mti uliokuwa pembezoni mwa jiko hilo kabla ya
kuwaua ndugu hao.
Shuhuda wa tukio hilo, Amina Tenge ambaye pia ni Ofisa Mtendaji wa
kijiji hicho, alisema waliwachukua ndugu hao na kuwapeleka Hospitali ya
Misheni ya Mchukwi kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya majeraha
waliyopata.
“Tulipofika hospitali walikuwa wameshafariki tayari,” alisema Tenge.
Mganga wa zamu wa Hospital hiyo, Esther Mtini aliwataja marehemu hao
kuwa ni Desteria Simba (40), Deborah Simba (2) na Amani Matimbwa (6).
Alisema baada ya kuifanyia uchunguzi miili hiyo, walibaini kuwa Desteria alikuwa ameungua kifuani, tumboni na shavuni.
“Amani aliungua tumboni na katika sehemu zake za siri na Deborah hakuwa na jeraha lolote,” alisema Dk Mtini.
Akizungumzia ajali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Nurdin Babu aliwataka
wananchi kuepuka kukaa chini ya miti au karibu na miti katika kipindi
hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha kwani ni hatari kwa maisha yao.
“Mvua hizi zinazoendelea kunyesha sasa zina madhara kwa sababu
zinaambatana na radi na upepo mkali, lazima tuchukue tahadhari kwa
kuacha kukaa chini ya miti au jirani ili kuepuka madhara yanayoweza
kutokea,” alisema Babu.
Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), juzi ilitoa tahadhari ya kuwapo kwa mvua
kubwa zinazoambatana na radi katika baadhi ya mikoa nchini, ukiwamo
Pwani
Tagged with: MATUKIO
Hakuna maoni :