Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua kulifuta kutoka katika Daftari la usajili wa magazeti, gazeti lijulikanalo kama “MAWIO”.
Amri ya kulifuta Gazeti hilo imetolewa leo 17 Januari, 2016
na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye
wakati alipokutana na Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Idara ya
Habari (MAELEZO) uliopo Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Nnauye amesema kuwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 55
lililotolewa tarehe 15 Januari, 2016 Serikali imelifuta Gazeti hilo
ikiwa ni uamuzi uliotolewa kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti Sura ya 229,
kifungu 25(1).
Alieleza kuwa, hatua ya kulifuta gazeti hilo inazuia pia
gazeti la Mawio kuchapishwa katika njia nyingine yoyote ikiwa ni pamoja
na mitandao (Online publication) kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya
Kieletroniki na Posta Sura ya 306.
‘’Serikali kwa masikitiko makubwa, imechukua uamuzi huu
kutokana na mwenendo wa uandishi wa gazeti hilo usioridhisha wa kuandika
na kuchapisha habari zenye mwelekeo wa uchochezi na kuhatarisha amani,
utulivu na usalama wa nchi yetu’’, alisema Nnauye.
Aidha, alifafanua kuwa hatua hiyo ya kulifuta gazeti hilo
imechukuliwa baada ya Msajili wa Magazeti kufanya juhudi kubwa za muda
mrefu kuanzia Juni, 2013 hadi Januari, 2016 kumtaka Mhariri wa gazeti
hilo kubadili aina ya uandishi wa habari na makala katika gazeti lake,
bila mafanikio.
"Msajili wa magazeti kwa juhudi zake alifanya
mawasiliano na Mhariri wa gazeti hilo mara nane kwa lengo la kutaka
afanye marekebisho ya mtindo wa kutoa habari zake lakini mhariri wa
gazeti hilo hakuzingatia ushauri mzuri aliopewa na Msajili wa Magazeti,
"Ninatoa wito kwa wamiliki, wahariri, waandishi na
watangazaji wa habari kuzingatia sheria, Kanuni na taratibu za taaluma
ya uandishi wa habari ambazo zikizingatiwa hakutakuwa na migogoro
yoyote.
"Aidha Serikali inasisitiza kwamba inaheshimu uhuru wa
vyombo vya habari unaozingatia maadili, weledi na Sheria za nchi na
kwamba Serikali itaendelea kushirikiana navyo’’ alisisitiza Mhe. Nnauye.
Katika hatua nyingine, Waziri nape alitoa pongezi kwa
Vyombo vyote vya habari nchini vinavyozingatia maadili, weledi na Sheria
zinazosimamia taaluma ya habari na sheria nyingine za nchi.
‘’Kwa namna ya pekee Serikali inawapongeza wamiliki na
wahariri wa vyombo vya habari ambavyo vinapofanya makosa vikielekezwa
hujirekebisha na kutoa ushirikiano kwa Serikali na pia kubadili mwenendo
wao; hawa ni pamoja na wahariri wa magazeti ya; Mwananchi Tanzania,
Mtanzania, The East African, Magazeti ya Daily News na Habari Leo, Uhuru
na mengineyo’’, alisema Mhe. Nnauye.
Hakuna maoni :